STRAIKA WA MWANASPOTI : Emery, Ole waamue moja kusajili au kusepa

Tuesday November 5 2019

 

By Boniface Ambani

Mambo yanazidi kuwa magumu kwa Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskajaer na Unai Emery wa Arsenal FC. Presha zinazidi kupanda kila wakati.

Hii ni kutokana na matokeo mabovu zinazopata klabu hizi yanayowakera mashabiki wao.

Nikianza na Man United, kipigo cha juzi jumamosi kutoka kwa Bournemouth FC kilikuwa ni aibu tupu kwani mara kwa mara imekuwa ikipoteza mechi zake kijinga kabisa.

Kinachokera zaidi mashabiki ni kuona washambuliaji wa United wakiwa ni vijana na wasio na uzoefu, hii ni ngumu kupata matokeo mazuri.

Wanaamini klabu yenye hadhi kama hiyo, haitakiwi kusuasua hivyo na kuonekana klabu ya kawaida sana.

Kutegemea washambuliaji kama Marcus Rashford, Antonio Martial na Jesse Lingard pekee ni aibu sana hasa baada ya kuondoka kwa Romelu Lukaku na Alexis Sanchez na kukosa wa kuziba nafasi zao. Hili lilinifanya nishangae sana uwezo wake kama kocha.

Advertisement

Ni wazi, Man United inahitaji wachezaji waliokomaa kisoka wenye kuweza kustahimili presha ambao wanakuwa kazi yao itakuwa kuwapa makinda hao uzoefu.

Kuwategemea makinda hawa ni sawa na kuchukua mashua kuvuka nayo bahari ya Hindi kutoka Afrika Mashariki na kati hadi Mumbai India. Haiwezekani. Mashua yako itapata tu gharika kabla hata ya kumaliza kilomita mbili.

Man United imecheza mechi 10 na wana alama 13, hii ni aibu, kwa kocha kama Ole nadhani ni kama amefika mwisho pale Old Trafford. Kuendelea kuwa na kocha kama huyu, ni kuharibu tu sifa ya United

Kwa upande wa Unai Emery, Arsenal kufungwa na kutoka sare kila kukicha ndio imekuwa utamaduni wao. Ni wiki mbili tu zimepita wametoka kutoka sare na Crystal Palace, pamoja na sare ya juzi na Wolves.

Inakera kwa timu kama Arsenal ambayo ina historia kubwa ya kushinda hasa mechi nyepesi kama hizi.

,Tatizo la klabu hizi mbili ni kukosa uelekeo kuanzia kwenye usajili ambao wengi waliona ni wakawaida sana kutokana na kujaza makinda.

Ni jambo jema kuwapa nafasi vijana lakini majukumu ambayo wamepewa ni makubwa kuliko walivyo.

Ni sawa na kumwachia mtoto mdogo0 alinde boma bila kumwelekeza la kufanya, hataweza. Kwa hivyo klabu hizi zinahitaji wachezaji wamekomaa. Asilimia 75 inafaa wawe wamekomaa kisoka kabisa. Asilimia 25 wawe hao wanaojifunza kutoka kwao.

Kitakwimu tu, asilimia 75 ya nyota wa timu hizi ni vijana chini ya umri wa miaka 24. Hapo unaoa sasa, ni ngumu kuweza kufanya mambo makubwa kuisaidia timu.

Embu jiuliuze, kwa nini klabu hizo zinacheza Europa League badala ya Ligi ya Mabingwa Ulaya waliko wanaume wengine wa shoka?

Pia angalia msimamo wa Ligi Kuu England.

Yote haya yanaakisi hali ya klabu hizi ambazo zimejaa makinda na wanaoonekana hawana ushindani wa kuwawezesha kushinda mechi.

Ziziachez tu Liverpool na Manchester City zizidi kutamba kutokana na kuwa na wachezaji wenye uzoefu. Kina Sadio Mane, Mohamed Salah, wa Liverpool, huku Kun Aguero, Raheem Sterling wa Man Man City.

Nyota kama hawa wanauzoefu na hata makinda walioko kwenye timu zao wanawasaidia sana kutokana na kupata uzoefu kutoka kwao.

Ndio maana nasema, tusudanganyane hapa, kuwategemea vijana tu kwenye kupata matokeo, jahazi litazama tu na hivyo ni kazi ya Ole na Emery kuamua kuondoka au wasajili wachezaji wenye uzoefu kwenye dirisha dogo la usajili la Januari ili kuondoa hizi aibu.

Advertisement