STRAIKA WA MWANASPOTI: Dua zetu tu, lazima nchi nne zifuzu Afcon 2019

Tuesday November 20 2018

 

By Boniface Ambani

Mechi za kuwania nafasi ya kushiriki katika mashindano ya AFCON, ziliendelea wikiendi hii iliyopita huku Uganda ikiwa ndio nchi ya kwanza kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki kukata tiketi ya kufuzu michuano ya aAfcon 2019 itakayofanyika Cameroon.

Cranes ambayo ipo katika kundi L ilifuzu fainali hizo, baada ya kuinyuka Cape Verde bao 1-0 mechi ambayo iliandaliwa katika Uwanja wa Nambole, Kampala. Uganda ipo katika kundi moja na Tanzania, Cape Verde na Lesotso na imefuzu fainali hizo kwa mara ya pili mfululizo ikiwa na alama 13, ikifuatiwa Lesotho na Tanzania zenye alama sawa, zote zina alama tano zikitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Cape Verde wanashika nafasi ya mwisho wakiwa na alama nne. Nikiangalia kwa karibu sana timu zote tatu zipo na nafasi sawa kabisa ya kufuzu. Tanzania itafuzu tu ikiwa itashinda mechi yao ya mwisho dhidi yao na Uganda.

Cape Verde wenyewe wakiishinda Lesotho na Tanzania ikose kupata ushindi dhidi ya Uganda wanafuzu. Tanzania nao wakishinda Uganda, huku Lesotho na Cape Verde zikose kufungana, basi Tanzania watafuzu.

Kwa hivyo, ni kundi ambalo lipo wazi kabisa kwa timu zote tatu. Hayo yatajulikana wakati mzunguko wa mwisho utapigwa mwakani.

Hayo yakijiri kundi la F linalo jumuisha Ghana, Kenya, Ethiopia na Siera Leone linabaki kuyumba kutokana na kifungo cha Siera Leone.

Siera Leone walifungiwa kutoshiriki katika mechi zozote zile na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), jambo ambalo linafanya kundi hilo kutojua hasa nini cha kufanya.

Hata hivyo, Kenya wanaongoza kundi hilo wakiwa na alama saba wakifatiwa kwa karibu na Ghana wakiwa na alama sita, huku Ethiopia nafasi ya tatu na alama nne.

Ni kundi ambalo halijulikani kulivyo lakini yote tisa, tunangojea uamuzi wa Shirikisho la Soka Africa, Caf. Inawatia kiwewe sana Wakenya kutokana na kuwekwa njiapanda na Fifa, hata hivyo, tuna imani ndani ya huu mwezi kila kitu kitakuwa kimeeleweka.

Nikiangalia kwa haraka haraka tu, Kundi la A. Senegal na Madagascar zimeshafuzu. Kundi la B. Morocco na Cameroon zimeshaafuzu. Kundi la C. Mali imeshafuzu. Vita vipo dhidi ya Burundi na Gabon. Burundi ikishinda mechi yao ya mwisho itafuzu.

Kundi la D. Algeria imeshapita na vita sasa ipo dhidi ya Benin, Gambia na Togo. Yeyote atakayeteleza hapo amepoteza.

Benin wana alama saba, Gambia na Togo alama tano kila mmoja na kinachosubiriwa ni mechi za mwisho kuamua.

Kwenye Kundi la E, The Super Eagles, Nigeria tayari bwameshafuzu na sasa kazi kubwa iko kwa Afrika Kusini na Libya huku ndizo zitakazocheza mchezo wa mwisho wa kuamua nani amfuate Nigeria, Afrika Kusini wakiwa na alama tisa huku Libya akiwa nazo saba. Kazi ipo Kundi la G. Hapa nafasi ipo kwa timu zote nne. Zimbabwe ina alama nane, Liberia saba, Congo sita na Congo DRC tano.

Kwenye Kundi la H, Guinea imeshafuzu huku Rwanda wakishindwa kufuzu. Ivory Coast iko nafasi ya pili na wanaweza kufuzu kwani wanahitaji alama moja tu.

Kundi la I, Mauritania imeshafuzu na sasa vita iko kwenye nafasi ya pili kati ya Angola wenye alama tisa na Burkina Faso wenye alama saba. Iwapo Angola atateleza na Burkina Faso apate ushindi, basi safari ya Angola itaishia hapo. Kundi la J limeshajulikana na timu za Egypt na Tunisia tayari zimeshafuzu zikiwa na alama 12 kila mmoja.

Kundi la K, Guinea Bissau ina alama nane, Namibia nane, Mozambique saba na Zambia alama 4.

Hapa kuna vita vikali sana huku Zambia ikiwa ameshabanduliwa na kuacha vita hiyo kwa wenzake.

Hata hivyo, tukirudi kwenye Kundi L na Uganda tayari imeshafika, kilichobaki kwa sasa ni kuziombea dua timu zetu zilizosaliaza ukanda huu ziweze kufuzu, ili angalau kwa mara ya kwanza ukanda huu uingize zaidi ya nne zifuzu.

Natumaini utajiunga nami kuombea timu zetu. Shukrani. Mungu akuzidishie.

Advertisement