Wolper, Ford, Lulu watarajia makubwa Cosota, Basata kuungana

Wednesday August 28 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Wacheza filamu, Jackline Wolper, Elizabet Michael (Lulu) na Shamsa Ford wamesema mpango wa kuunganisha vyombo vya kusimamia sanaa nchini vya Cosota, Basata na Bodi ya Filamu vitachangia kurudisha tasnia hiyo kwenye kiwango bora.

Wasanii hao ni miongoni mwa waliojitokeza kwenye mkutano wa Waziri wa habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na mwenzake wa Viwanda na biashara, Innocent Bashungwa.

Mkutano huo wenye ajenda mbili ikiwamo ya kuona ni namna gani Taasisi hizo tatu zinavyoweza kufanya kazi kwa pamoja sanjari na wasanii kupata gawio (mrabaa) kutokana na kazi yao.

Wakizungumza katika mkutano huo wasanii hao walisema jambo hilo walitamani lifanyike muda mrefu na limekuja wakati muafaka.

"Tukiwa kitu kimoja hata sheria kali zitapunguzwa, lakini pia umoja ni nguvu, hatuwezi kusimamisha Tasnia kama hatuna umoja," alisema Wolper.

Alisema kitendo cha kuwa na matabaka wakati wote wanafanya kazi ya sanaa kinapunguza msisimko hivyo wakiwa kitu kimoja sanaa itapiga hatua.

Advertisement

Shamsa alisema anategemea mambo mazuri katika mkutano huo kwani unalenga kumaliza changamoto ambayo walitamani itatuliwe muda mrefu.

"Mkutano huu ni wa kutujenga na kutoka sehemu moja kwenda nyingine, baada ya kongamano hili tutakuwa na hatua na kupigakwa kila msanii, lakini tatizo jingine ni kwa wasambazi, kama wakipatikana 10 tu ambao hawatunyonyi, wasanii tutatoka hapa tulipo na kufika mbali," alisema.

Elizabeth Michael ‘Lulu’ alisema yuko tayari kuchangia mawazo, muda na nguvu kuhakikisha kile ambacho kitapeleka tasnia mbele.

Alisema hana utaalamu wa hizo taasisi kuunganishwa, lakini zikiwa taasisi moja kutakuwa na urahisi wa mambo mengi, japo wataangalia faida na hasara zake.

Upande wa Ado Novemba yeye alikuwa tofauti akitaka Cosota iwe na nguvu peke yake huku Bodi ya Filamu na Basata ndizo ziunganishwe.

"Cosota ni haki mmiliki ambayo kama mtu amegundua kitu chake basi anakuwa na haki miliki, tuwape nguvu Cosota wafanye kazi ipasavyo kama Taasisi inayojitegemea," alisema Ado.

 

Advertisement