Wema Sepetu anafunga mwaka akijutia ishu ya mapenzi

Muktasari:

Wema, ambaye aliingia matatani na vyombo vya kisheria kutokana na ishu za mapenzi, ameliambia Mwanaspoti kuwa alikuwa anapenda kumweka hadharani kila mwanamume anayetoka naye kimapenzi, lakini tabia hiyo haikuwa na manufaa kwake zaidi ya kumharibia ikiwemo watu kumhesabia idadi ya wanaume anaotoka nao pindi tu wanapoachana.

STAA wa kike wa Bongo Movies, Wema Sepetu a.k.a Madame amesema anajutia sana kuweka wazi uhusiano wake wa kimapenzi, lakini sasa anakwenda kufunga mwaka na mabadiliko makubwa kitabia.

Wema, ambaye aliingia matatani na vyombo vya kisheria kutokana na ishu za mapenzi, ameliambia Mwanaspoti kuwa alikuwa anapenda kumweka hadharani kila mwanamume anayetoka naye kimapenzi, lakini tabia hiyo haikuwa na manufaa kwake zaidi ya kumharibia ikiwemo watu kumhesabia idadi ya wanaume anaotoka nao pindi tu wanapoachana.

“Huwezi amini najutia sana tabia niliyokuwa nayo, huwa napenda kumweka hadharani mwanamume nitakayekuwa naye nikiamini ni kumuonyesha nina mapenzi ya kweli. Lakini, kumbe nilikuwa nafanya ujinga ambao hauna faida kwa watu zaidi ya kukuhesabia wanaume uliotoka nao. Sasa unawajulisha watu ili iweje? Mie sasa hivi sitaki hayo mambo na nimebadilika na ninaye mpenzi lakini hakuna anayemjua,” alisema akisema tabia hiyo imemfunza mengi.

“Mwaka huu kuna mambo mengi ya maana nimefanya kwa ajili ya maisha yangu, lakini kuna mabaya pia ambayo yamenipa funzo na kunifanya nijifunze kutokana na makosa. Bado nasali sana ili Mungu anipe uwezo wa kuishinda tabia ya kutangaza wanaume mitandaoni na hila naona ninakwenda kufanikiwa kwani, mwaka unamalizika nikiwa na mambo mazuri,” alisema Wema.