Warembo wa Vyuo Vikuu wachomoza

Muktasari:

  • Kahabuka alisema lengo la shindano la Miss Utalii ni kupata mabalozi watano wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Morogoro.

Morogoro. Warembo 35 wa Vyuo Vikuu vinne wanatarajiwa kuchuana kuwania taji la Miss Utalii 2018, likalofanyika Desemba 22 mkoani hapa.

Washiriki wanaotarajiwa kupanda jukwaani wanaotoka Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA), St Joseph Kihonda, Mzumbe na St Jordan.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Kituo cha Taarifa za Utalii, Samson Kahabuka alisema kuwa mrembo atakayeibuka mshindi atapata ajira katika kituo hicho.

Kahabuka alisema lengo la shindano la Miss Utalii ni kupata mabalozi watano wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Morogoro.

“Mkoa wa Morogoro una vivutio vingi vya utalii ambavyo havijapata fursa ya kutangazwa, ujio wa shindano hili ni kupata mabalozi watakaotangaza vyema vivutio hivyo,”alisema Kahabuka.

Mmoja wa washiriki wa shindano hilo, Joaniter Ernest alisema endapo ataibuka mshindi atatumia fursa hiyo kutangaza vivutio vya Mlima Udzungwa.

Mrembo huyo alisema milima ya Udzungwa ina vivutio vingi ikiwepo aina 11 ya nyani zikiwemo tano ambazo hazipatikani sehemu yoyote duniani.

Naye Berita Mdachi alisema atatumia nafasi hiyo kutangaza utalii wa mkoa huo kwa sababu baadhi ya vivutio havijulikani kwa kuwa havitangazwi huku jamii ikiamini Arusha ndiyo mkoa wenye vivutio vingi nchini.

Kiongozi wa warembo hao, Neema Mathayo alisema washiriki wataingia rasmi kambini leo kujiandaa na shindano hilo.