Warembo wa 'Miss Tanzania' wana jambo lao Novemba 14

WAREMBO waliowahi kutwaa taji la Miss Tanzania kwa nyakati tofauti wameamua kujitoa kwa jamii kwa kujikita kusaidia wanawake na watoto wenye uhitaji.

Warembo hao wakiongozwa na Miss Tanzania wa mwaka 2000, Jackline Ntuyabaliwe watakutana Novemba 14, 2020 kwenye hoteli ya Hyatt, Dar es Salaam katika tukio la kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia jamii.

Akizungumza leo Jumanne, Septemba 29, 2020 jijini Dar es Salaam wakati wa kuzindua mpango huo uliopewa jina la Beauty Legacy Tanzania, Jackline amesema wameamua kujitoa kwa jamii kama ambavyo moja ya misingi ya shindano hilo linaelekeza.

"Kwenye Miss Tanzania hadi Miss World kuna kipengere cha kusaka mrembo mwenye malengo, kuwa mrembo tu haitoshi, hivyo tunawajibu kufanya kitu kwa jamii," amesema Jackline ambaye aliambatana na Happiness Magese, Genevive Mpangala, Nancy Sumari na Queen Elizabeth.

Amesema amepata wazo la kuwakutanisha warembo wote waliowahi kutwaa taji la Miss Tanzania ili kufanya jambo hilo.

"Novemba 14 wote watakuwepo katika hafla hii kwa ajili ya kuchangia fedha za kusaidia jamii yenye mahitaji, hususani mama na watoto," amesema.

Amesema wanalenga kusaidia wodi za wajawazito, kujenga maktaba za watoto kwenye hospitali na kuwasaidia watoto wanaozaliwa kabla ya muda 'njiti'.

"Katika event yetu tutazialika kampuni, taasisi, mashirika na watu mbalimbali, watashiriki kwa kununua meza," amesema ingawa amesisitiza kuwa hawana kiwango rasmi cha fedha wanazohitaji kukusanya.

"Tukipata fedha nyingi ndivyo tutaweza kuwafikia wahitaji na kuwasaidia kote nchini kwa kiwango kikubwa," amesema.

Miss Tanzania huyo amesema hivi sasa wako katika mchakato wa kutafuta wadhamini ili kufanikisha tukio hilo.

"Mwaka huu nafikisha miaka 20 tangu nilipotwaa taji la Miss Tanzania, hivyo niliona niwashirikishe na warembo wengine waliowahi kutwaa taji hilo ili kwa umoja wetu tufanye kitu katika jamii.

"Wote walilipokea suala hili vizuri na tutakutana kwa mara ya kwanza warembo wote Novemba 14," amesema.

Kwa nyakati tofauti, warembo baadhi wa Miss Tanzania walioambatana na Jackline kwenye uzinduzi wa tukio hilo, walimpongeza Miss Tanzania huyo kwa kufanya jambo ambalo limewakutanisha pamoja na kujitoa kusaidia jamii.

S.Shindano la Miss Tanzania limekuwa likifanyika kila mwaka tangu mwaka 1994 lilipirejeshwa upya nchini hadi mwaka 2019, ingawa mwaka huu halijafanyika kutokana na janga la corona.

 

"