Wanamuziki wanaofunga mwaka kwa ngoma kali

Muktasari:

  • Mwaka ukiwa unaishia wasanii baadhi wameachia ngoma ambazo zimekuwa kama ni fungia mwaka kwa upande wao na mashabiki.

Dar es Salaam. Mwaka unaelekea ukingoni ni muda ambao kila mmoja anakuwa anaangalia amefanya nini tangu mwanzoni mwa mwaka, wakati huo huo huo wengine wanaangalia namna ambavyo wanaweza kufunga mwaka wao vizuri.
Mwanaspoti limeangalia namna ambavyo wasanii kadhaa walivyoufunga mwaka huu kwa kuachia ngoma kali ambazo zinaacha alama kwa mwaka huu unaelekea ukingoni.


RICH MAVOKO
Msanii huyu ambaye alikuwa katika kundi la Wasafi aliondoka katika kundi hilo huku kukizua maneno mengi juu ya kuondoka kwake ni kama amepotea katika mziki.
Lakini alituliza akili na kujua amekosea sehemu gani na kisha alifanya maamuzi kwa kutoa ngoma ‘Ndegele’ na ‘Wezele’ ngoma ambazo zimekuwa kali na kufungia mwaka.
Uwezo wake wa kutunga mistari ndio umemfanya aweze kutuliza akili kwa haraka na kufanya ngoma hizi ambazo kwa namna moja ama nyingine zimemuingiza katika orodha ya wasanii waliofunga mwaka vizuri.


ALIKIBA
Alikuwa ni msanii mzito katika kuachia nyimbo lakini hivi sasa imekuwa tofauti kutokana na kwamba ameamua kufunga mwaka kivingine kabisa kwa kuachia nyimbo.
Kiba safari hii yeye na kundi lake la Kingsmusic wameachia ngoma kama ‘Toto’ huku wasanii ndani ya kundi hilo nao wakiachia wimbo ‘Masozy’ na yeye mwenyewe kuamua kuachia ngoma ya ‘Kadogo’.
Wakati ngoma ya kadogo ikiwa inafanya vizuri, msanii huyo bado amepanga kufunga mwaka kwa kufanya shoo yake binafsi, wakati huo huo akipanda katika jukwaa la Fiesta licha ya kwamba mwanzoni ilishindikana kupanda baada ya kuwa na shoo zake lakini Fiesta ilishindikana kufanyika na sasa itafanyika tarehe 22 na yeye akiwepo.


SHETTA
Msanii huyu ambaye aliwahi kutamba na ngoma ‘Nimechokwa’ aliyofanya na Bele 9, alitamba na ngoma nyingi mno ambazo zilimsogeza katika mziki na kuzidi kujulikana mpaka nje ya mipaka ya Tanzania.
Hata hivyo baadae ukaja ukimya mkubwa kwake na wengi wakijiuliza amekaa upande upi, kumbe kimya chake kina mshindo kwani ameibuka na kuachia ngoma ya ‘Hatufanani’ aliyowashirikisha Jux na Mr Blue.
 Ngoma hii imekuwa kali na ilivyotoka kila mpenda mziki mzuri alifurahishwa na urejeo wa msanii huyu hasa katika upande wa Jux ambaye ametambaa vizuri katika kiitikio cha ngoma hiyo iliyopendezeshwa na michano mikali ya Mr Blue.


WASAFI
Kundi hili wasanii wake wote moja kwa moja wameufunga mwaka kivingine kutokana na kwamba wamekuwa wakiachia ngoma ambazo zimekuwa zikitazamwa sana kwenye mitandao (Trending).
Rayvanny na Diamond waliachia ngoma ya ‘Nyegezi’ ambayo ilizua gumzo kutokana na mashairi yaliyoimbwa lakini hata hivyo ikaja kugeuka nyimbo ambayo inasikilizwa na kutazamwa mara nyingi.
Wakati huo huo; Harmonize na Rayvanny nao wamekuja kuachia ngoma kali ya Paranawe ambayo imekuwa kama funga mwaka kutokana na mashairi ambayo wameyatunga.
Wimbo ambao unachezeka na unasikilizika na kuwafanya watu wanaopenda mziki mzuri kupata muda wa kuusikiliza mara kwa mara na kupigwa katika kumbi za starehe.


NAVY KENZO
Kundi hili kwanza ni wapenzi ambao wamedumu kwa muda mrefu katika mahusiano yao. Maisha ya mziki na maisha ya kawaida wameweza kuyaweka pamoja na maisha yameendelea.
Baada ya kupata mtoto wengi walitegemea kuona labda wanaweza wakatulia ili kuachia ngoma, lakini kilichotokea ni kwamba waliachia ngoma ‘Katika’ wakimshirikisha Diamond ngoma ambayo imetamba na imekuwa kama ya kufungia mwaka kwa upande wao.


DARASA
Wengi walikuwa wakisema kwamba msanii huyu alijiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya, ukweli alipotea na kukaa kimya kwa muda mrefu na ndipo maneno yalizidi kukua.
Lakini kabla ya mwaka haujamalizika, Darasa ameamua kufunga mwaka kivingine kwa kuachia ngoma mbili za ‘Tofauti’ na ‘Achia njia’ ambazo mapokeo yake yamekuwa mazuri.
Uwezo wake wa kuchana kwa staili yake ya kipekee umemfanya mashabiki wampokee kwa mikono miwili lakini pia kwa ukimya wake wa muda mrefu walimis mistari yake.


YOUNG KILLER
Msanii huyu tangu aingie katika lebo ya Wanene Entertainment, amekuwa akiachia nyimbo mfululizo kwani aliachia ‘Secreto’ hata hivyo haikutamba.
Hivi sasa ameachia nyimbo kali ya kufungia ‘Sinaga Swaga 3’ ambayo mapokezi yake yamekuwa makubwa kuanzia katika vituo vyote vya runinga na redio mpaka katika upande wa mitandao ya kijamii.