Wajanja waliojimilikisha pisi kali za Kenya

LINAPOKUJA suala la mahaba, mastaa wengi wa kiume wa Bongo wanaonekana kunasa kwa urahisi kwenye ulimbo wa mademu kutoka nchi jirani. Harmonize ana demu wa Kitaliano, Jux alikwenda China kusoma akahitimu na demu wa Kifilipino, Linex alikuwa na pisi ya kizungu kutoka Finland na listi inaendelea. Jamaa hawana mchezo.

Lakini, licha ya kuwa pisi kali za nje zinawindwa sana na wasanii wa Bongo, inaonekana ni kama vile windo jepesi zaidi kwa mabraza ni hapo nchi jirani ya Kenya. Na ili kuthibitisha hilo, hii hapa listi ya mastaa wa kiume kutoka Bongo waliowahi kuthibitika kuwa na mabebi kutoka Kenya.

A.Y

Kabla ya kufunga ndoa na mkewe kutoka Rwanda anayeitwa Remy, mzee wa komesho aliwahi kunasa kwa msanii kutoka Kenya, Cecilia Wairimu maarufu Amani. Na za chinichini zinasema ilibaki kidogo tu wawili hawa wawe mke na mume kabla ya jini mkata-kamba kuingia kati na kuvuruga mipango.

AY na Amani walikutana mwaka 2005 huko huko Kenya, ambapo kwanza walikuwa marafiki kisha wapenzi kabla ya 2007 kupigana kibuti, huku sababu ikitajwa kuwa ni umbali na gharama za kuhakikisha penzi hilo linafanya kazi.

“Mimi sikuwa tayari kuhamia Kenya, naye hakuwa tayari kunifuata Tanzania. Kwa hiyo umbali ulifanya tushindwe kuwa pamoja.” alieleza A.Y kwenye mahojiano na chombo kimoja cha habari.

Baada ya mahusiano hayo Amani aliibukia kwenye mahusiano mengine ambayo kwa sasa yamekuwa ndoa, wakati A.Y pia alifunga ndoa 2018 na mrembo kutoka Rwanda na kwa sasa wana mtoto mmoja.

BEN POL

Ijumaa wiki iliyopita Ben alibadilisha dini kuwa muislam, lakini kabla ya hapo zilisambaa picha zikimuonyesha yeye na mpenzi wake mfanyabiashara kutoka Kenya, Anerlisa Muigai wakifunga ndoa kanisani, hii inamaanisha kuwa huenda ndoa hiyo ilishavunjika.

Arnelisa na Ben walikutana mwaka 2018 Kenya ambapo, Ben alikwenda kikazi. Akisimulia Ben ambaye jina lake la kiislamu ni Benham anasema;

“Nilikuwa Kenya kikazi tukakutana kwenye mkutano wa waandishi wa habari ulioandaliwa na rafiki yake! Nilikuwa simfahamu lakini yeye alikuwa ananijua. Tukaongea na tukabadilishana namba na mengine yakafuata,” anasema Ben.

Baada ya uhusiano kunoga Ben alibeba mabegi yake na kwenda kuishi Kenya kwa muda mrefu. Na kwa kipindi chote hicho alipotea kwenye gemu kwa maana ya kwamba, alikuwa hatoi ngoma kwa kasi yake ya zamani na hata ngoma chache alizokuwa anatoa alikuwa hazitangazi vilivyo.

ALIKIBA

King Kiba ana watoto wanne na watoto watatu wa kwanza amezaa na wanawake kutoka Tanzania… lakini alipoamua kuoa alikwenda zake Mombasa, Kenya na kuchukua kimwana Amina bint Khalef.

Ndoa yao ilifungwa mwaka 2018 kwa usimamizi wa karibu wa Gavana wa Mombasa, Hassan Joho, lakini 2019 ziliibuka tetesi kwamba wameachana eti kwa sababu Amina alishindwa kuishi kwa Alikiba kutokana na madai kibao ila jamaa akasisitiza ndoa yake iko freshi.

Hata hivyo Septemba 2020, Alikiba kupitia kwenye mahojiano na chombo kimoja cha habari nchini alithibitisha kwamba, hakuwahi kuachana na mkewe wala kuwa na mgogoro kama idaiwavyo.

Ndoa ya Kiba na Amina imetoa matunda ya mtoto mmoja wa kiume, Keyaan.

DUMA

Jamaa ni muigizaji, amecheza kwenye tamthilia kama vile Siri ya Mtungi, filamu ya Nipe Changu, Bei Mbaya na zingine.

Kwa takriban mwezi sasa amekuwa akimiminisha picha zinazo muonyesha yeye na mpenzi wake ambaye ni muigizaji kutoka Kenya, Mishi Dora.

Kwa mujibu wa Duma, yeye na Mishi walikutana Mombasa, Kenya miaka mitatu iliyopita alipokwenda kucheza kwenye filamu moja iliyotengenezwa huko. Na hata kwenye filamu waliigiza kama mke na mume.

“Mimi na yeye tulikuwa tunaigiza kama mke na mume kwenye filamu hiyo. Tukaona kama ‘chemistry’ zetu zinaendana hivi, hivyo tukaamua kwanini isiwe kweli. Na sasa tuko hapa.” alisema Duma.

DIAMOND

Tungemaliza listi hii bila jina la Diamond hata mimi ningeshangaa kwa sababu linapokuja suala la mademu jamaa ni kama anatafuta ubalozi, ana listi ndefu.

Lakini, pisi iliyomuingiza kwenye listi hii inaitwa Tanasha Dona. Mwanamuziki ambaye pia ni video vixen kutoka Kenya.

Kwa mujibu wa Tanasha alisema yeye na Diamond walikutana club Kenya kipindi ambacho Mondi alikuwa akidate na Zari, wakabadilishana namba, lakini wakapotezana kwa muda wote huo mpaka mwaka 2018 walipokutana tena.

Kwa sasa wawili hawa hawako pamoja lakini wamebarikiwa mtoto mmoja wa kiume, Naseeb Junior. Penzi la Tanasha na Diamond liliguwa gumzo kinoma huku supastaa huyo wa Bongo Flava akifichua kwamba, mrembo huyo ni mwelewa sana.

WENGINE

Muimbaji kutoka Tanga ambaye alisumbua sana kwenye game, Hussein Machozi anadaiwa kuwa alifunga ndoa na mwanamke kutoka Kenya, Shuena. Hata hivyo, baadaye mambo kibao yakaibuka.