WCB wafunguka ishu ya Diamond kupigwa chupa

Kama ni mfuatiliaji katika mitandao ya kijamii, moja ya habari iliyoteka mitandao hiyo jana na leo ni sakata la msanii Diamond Platnumz kurushiwa chupa akiwa kwenye shoo nchini Malawi.

Diamond amekuwa nchini humo mwishoni mwa juma lililopita kwa ajili ya show ambayo alikuwa aifanye siku ya Jumamosi.

Hata hivyo siku hiyo ilipofika alishindwa kutumbuiza na kutupia taarifa katika ukurasa wake wa Instagram kuwa sababu za kushindwa kufanya hivyo ni kutokana na kunyesha mvua kubwa.

Jana Novemba 2, 2020 kulisambaa video kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha mashabiki wakiwa wanarusha chupa katika jukwaa ambalo Diamond alipaswa kupanda na kuzua maswali mengi kuwa ilikuwaje wakafikia hatua hiyo.

Mwanaspoti limeutafuta uongozi wa WCB na kufanikiwa kuzungumza na mmoja wa mameneja wa lebo hiyo, Sallam Shariff.

Akielezea mkasa mzima, Sallam amesema katika shoo aliyokwenda Diamond, lilikuwa ni tamasha la siku tatu lililoanza tangu siku ya Ijumaa Novemba 30.

“Wakati tamasha hilo lilianza siku ya Ijumaa, ratiba ya Diamond kupanda jukwaani ilikuwa Jumamosi, lakini kutokana na kunyesha kwa mvua kubwa muda ambao msanii wetu alipaswa kupanda jukwaani ilishindikana,”

“Kulikuwa na wasanii wengine wa nchini humo wakiendelea kutumbuiza, hivyo mashabiki wakaanza kurusha chupa kulazimisha kutaka kumuona Diamond akipanda kuimba, hicho ndicho kilichotokea ndugu mwandishi na sio hivyo vinavyozungumzwa mitandaoni, “amesema Sallam.

Pamoja na changamoto hiyo, meneja huyo amesema Diamond alifanikiwa kufanya show kubwa siku ya Jumapili usiku.

Akizungumzia kuhusu video ya Diamond akionekana kukasirikia na kuelekea hotelini inayosemekana kuwa ni baada ya kurushiwa chupa, Sallam amesema “Pale alikuwa akishuti kwa ajili ya tangazo la kufanya show hiyo kesho (Jumapili) baada ya mvua kumuangusha siku ya Jumamosi,”