Vee Money,Rotimi ni maswali kibao huko mtandaoni

Muktasari:

Staa huyo wa kike amezoeleka kuwa ni mtu msiri linapokuja suala la mahusiano na hata kipindi wanaanzisha uhusiano na Jux ilichukua muda mrefu kuthibitisha kwamba, ni wapenzi kwani kila wanapulizwa huyakana.

KUTOKANA na mapicha picha na video za kimahaba kutoka kwa supastaa wa kike wa Bongo Fleva, Vannesa Mdee na mwigizaji wa Marekani mwenye asili ya Nigeria, Rotimi kuzagaa huko mtandaoni, waendesha mashitaka na mashahidi wa huko Instgram kila mmoja anasema lake.

Kila mmoja amepatwa mshangao akijaribu kumwelezea V-Money kwa namna anavyomjua huku wengi wakisema amekuwa na mabadiliko makubwa. Mabadiliko hayo yanatokana na ukweli kwamba, Vanessa hakuwa mtu wa kujiachia sana linapokuja suala la mapenzi kama ilivyo sasa, ambapo video na mapichapicha kama yote huko mitandaoni.

Staa huyo wa kike amezoeleka kuwa ni mtu msiri linapokuja suala la mahusiano na hata kipindi wanaanzisha uhusiano na Jux ilichukua muda mrefu kuthibitisha kwamba, ni wapenzi kwani kila wanapulizwa huyakana.

Taarifa za Vannesa na Rotimi kutoka kimapenzi zimeanza kushika kasi mwezi Novemba na wenyewe hawakuchukua muda kukiri kwamba, ni wapenzi tofauti na ilivyokuwa kwa Jux.

Juzi kati Rotima alikuwa alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ambapo, Vanessa aliitumia kushiriki naye bega kwa bega ikiwa ni pamoja na kushusha mavideo na mapicha kibao kuelezea hisia zake kwa mchezaji filamu huyo, ambaye ni miongoni mwa mastaa wa filamu wanaotesa huko Marekani kwa sasa.

Picha na video hizo ndio zikaongeza joto huko Insta ambapo, kila shabiki alishindwa kuficha hisia na kudondosha maoni huku wengi wakimpongeza kwa kuchukua uamuzi sahihi baada ya kutemana na Jux.

Mwanaspoti limemsaka Vannesa na kupiga naye stori ambapo, alikiri kuwa kweye uhusiano na Rotimi huku akifunguka kwamba, anajiachia kutokana na staili ya maisha yake na mpenzi wake huyo.

“Unajua katika mapenzi kuna mambo mengi sana na moja ni jinsi mlivyozoeshana...yaani staili yenu ya maisha ya mtu na mpenzi wake. Kwa Jux sikuweza kuishi na staili hii ya kujiachia kwa sababu hatukuzoeshana kujiachia mitandaoni kama hivi.

“Kwa maana hiyo sioni sababu ya watu kudai kuwa namringishia Jux baada ya kuachana ama bado nina stress kwa kuwa, bado namhitaji,” alisema Vanessa ambaye kwa mara ya kwanza walikutana na Ritimi kwenye tamasha la Essence lililofanyika New Orleans, Marekani.

Katika tamasha hilo, Vanessa na Rotimi, ambaye pia ni mwamumizi wote walikuwa na mwaliko wa kutumbuiza na hapo kila mmoja akanasa kwenye rada za mwenzake na hasi sasa mambo ni mambo.