Usiku wa Sikinde ilikuwa balaa

Muktasari:

  • Onyesho hilo la kuadhimisha miaka 40 tangu bendi hiyo ilipoasisiwa mwaka 1978, lilifanyika kwenye Uwanja vya Bandari, Tandika jijini Dar es Salaam na kubamba kinoma.

NANI aliyekuambia dansi hasa la bendi kongwe limekufa? Waulizeni waliohudhuria onyesho maalumu Wakongwe Mlimani Park ‘Wana Sikinde’ iliyofanyika juzi Jumamosi.

Onyesho hilo la kuadhimisha miaka 40 tangu bendi hiyo ilipoasisiwa mwaka 1978, lilifanyika kwenye Uwanja vya Bandari, Tandika jijini Dar es Salaam na kubamba kinoma.

Kuna mashabiki waliotimba kama kutaka kusanifu tu dansi linakuwaje, lakini kile walichokutana nacho ikiwamo mizuka ya wanazi wa muziki huo uliwaacha midomo wazi.

Utamu wa onyesho hilo ulichombezwa na dansi matata lililoporoshwa na wakongwe hao wakianikizwa na sauti tamu za kina Hassan Bitchuka na wenzake.

Kali zaidi ni kolabo waliyopata kutoka kwa Bogoss Band chini ya Nyoshi El Saadat aliyewafanya mashabiki kutokaa vitini kwa muda wote wa burudani hiyo iliyotia fora jijini.

Utamu ulivyoanza

Bogoss Musica ilianza kupanda mapema saa 10 jioni na kutumbuzia kwa shoo bab’kubwa iliyowapagawisha mashabiki waliofurika uwanjani hapo bila kutarajiwa.

Bendi hiyo mpya ilianza na wimbo wao wa ‘Anna’ kisha likafuata sebene la nguvu la dakika tatu kabla ya kuimba ‘Mama wa Kambo’ wenye rapu ya Naliamsha Dude.

Utamu wa kibao hicho uliwafanya mashabiki kumlazimisha MC wa shughuli hiyo, Rajabu Zomboko, kuitaka Bogoss irudie tena wimbo huo.

Achana na mpangilio wa vyombo na sauti za waimbaji wa bendi hiyo, mashabiki walipagwa na shoo kabambe ya madansa wao walioshambulia jukwaa bila kuchoka.

Shoo ya Bogoss iliendelea hadi saa 2:30 usiku wakati wenye shughuli walipopanda jukwaani kuliamsha dude.

Kabla Sikinde kuwasha moto walianza kwa kupasha moto vyombo kwa nusu sasa na kuibua minong’ono kwamba Bogoss huenda ikaachwa solemba na wakongwe hao.

Ndipo saa 3 usiku kazi ikaanza rasmi kwa wimbo wa Wikiendi kama kete ya kwanza ikiwa ni kati ya nyimbo za mwanzo kabisa za bendi hiyo kwa mwaka 1978.

VIGONGO

Baada ya Wikiendi Sikinde iliendelea kuangusha moja baada ya nyingine na kuwafanya vijana wa zamani kukumbushwa mbali, huku mayanki wa sasa wakishuhudia utamu waliokuwa wakiusikia tu Redio Tanzania enzi hizo.

Nyimbo kama Maudhi ya Kila Siku, Usitumie Pesa, Kiguu na Njia, Naisubiri Bahati na nyingine kuwakuna wengi hasa sauti tamu isiyochuja ya Hassan Rehani Bitchuka.

Bitchuka aliwakuna wengi hasa alipoimba nyimbo za Clara, Hiba na Fikirini na nyingine zilizoipa ujiko mkubwa Sikinde kiasi cha kuwa Mabingwa wa Dansi Tanzania.

Sikinde pia ilipiga nyimbo zao mpya ambazo ziliwapa burudani ya aina yake mashabiki walioshindwa kujizuia na kujimwaya uwanjani kuserebuka kwa raha zao.

NYOSHI ASHINDWA KUJIZUIA

Wakati Sikinde ikiwa jukwaani Nyoshi El Saadat, alipanda jukwaani na kuomba kuimba wimbo wa Hiba na kuimba sambamba na waimbaji wa bendi hiyo akiwamo Bitchuka.

Nyoshi alikiri wazi licha ya kuwa na sauti nyororo, lakini kwa Bitchuka alimvulia kofia kwani, alisema haifikii hata kidogo na kumsifu kwa kuitunza hadi leo.

Katika burudani iliyowasisimua wengi ni mngurumishaji wa gitaa zito la besi, Tony Karama, kwa namna alivyokuwa akilitia madoido, huku wapiga gitaa wengine nao wakiacha gumzo kwa mashabiki.

SHAABAN LENDI

Mbali na wapigaa magitaa, lakini mkongwe mwingine aliyewashangaza watu ni Shaaban Lendi anayepuliza midomo ya bata (saxaphone).

Licha ya uzee aliokuwa nao, lakini Mzee Lendi alionekana bado ni mahiri akisaidiana na wenzake katika kupuliza ala za upepo wa bendi hiyo.

Lendi alianza manjonjo yake katika kibao Rama Mzazi Mwenzangu kilichoimbwa enzi hizo na waimbaji Fresh Jumbe Mkuu, Bennovilla Anthony na Francis Lubua.

WENGINE WALIKACHA

Licha ya awali kuelezwa kuwa wakongwe wa zamani wa bendi hiyo ambao walishaachana na Sikinde wangekuwepo, lakini wengi wao hawakuonekana.

Wanamuziki waliotajwa wangeliamsha dude pamoja na wenzao ni Fresh Jumbe Mkuu, aliyepo Japan kwa sasa, Bennovilla aliyepo Super Kamanyola ya Mwanza na Cosmas Chidumule anayeimba nyimbo za Injili hawakuwapo.

Wengine ni Hussein Jumbe, Henry Mkanyia na wengine, huku Max Bushoke licha ya kuchelewa lakini alifika ukumbini akitokea moja kwa moja Uwanja wa Ndege akitokea Afrika Kusini na kuungana na wenzake.

GAMA KAMA KAWA

Mkali wa gitaa la kati (rhythm) Abdallah Gama naye alikuwapo ukumbini hapo na kupanda jukwaani kutambulishwa sambamba na wenzake.

Gama anakumbukwa kwa umahiri wake na kazi kubwa aliyoufanya kwenye nyimbo za bendi hiyo, hasa kibao cha Gama kuilichotungwa na Tshimanga Kalala Assosa na mkali huyo kukifanyia kazi kwa kiwango cha hali ya juu.

Mpaka onyesho linafikia tamati saa 6 usiku kila aliyekuwa uwanjani hapo aliondoka akiwa amesuuzika na kuimwagia Sikinde na hata Bogoss kwa kazi kubwa waliowafanyia.