Upelelezi umekamilika kesi ya Wema kuunguruma Februari 21

Muktasari:

 

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Februari 21, mwaka huu kumsomea Maelezo ya Awali (PH) Miss Tanzania wa zamani Wema Sepetu.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Februari 21, mwaka huu kumsomea Maelezo ya Awali (PH) Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa shauri hilo kukamilika na hivyo upande wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo ipange terehe kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa huyo, Maelezo ya awali.

Wema anakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha video ya ngono na kusambaza katika mitandaoni ya kijamii.

Wakili wa Serikali, Glori Mwenda, ameieleza mahakama hiyo leo Jumatano, Februari 13, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonda, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

"Shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa na taarifa njema ni kwamba upelelezi wa shauri hili umekamilika, hivyo tunaomba tarehe kwa ajili ya kumsomea Maelezo ya awali, mshtakiwa huyu," amedai Mwenda.

Hakimu Kasonde baada ya kusikiliza Maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 21, mwaka huu ambapo upande wa mashtaka utamsomea PH.

Wema ambaye anatetewa na wakili, Ruben Simwanza, alifikishwa kwa mara ya kwanza Kisutu, Novemba Mosi, 2018, kujibu shtaka hilo.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana.

Katika kesi ya msingi, Wema anadaiwa Oktoba 15, 2018 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam alichapisha video ya ngono na kuisambaza katika mtandaoni wake wa kijamii wa Instagram.