UWOYA: Bila janjaro naishije sasa, mtasubiri sana

Friday September 14 2018

 

By RHOBI CHACHA

KWA sasa ukiuliza habari ya mjini kwa upande wa mastaa wa kike wa Bongo, anayefunika kwenye mavazi utajibiwa ni mwigizaji wa Bongo Movie, Irene Pancaras Uwoya.

Uwoya amekuwa kivutio katika Mtandao wa Instagram kwa mwonekano wake wa kutupia nguo ambazo hajawahi kuonekana nazo, hivyo ameibua minon’gono kwa mashabiki kuwa ndiye staa wa kike anayeongoza kuvaa nguo zenye mvuto na za gharama tofauti na hapo mwanzo.

Awali, aliyekuwa akifunika kwa mavazi kwa wasanii wa kike alikuwa ni Madam, Wema Sepetu.

Fununu zinadai huenda Uwoya amenyooshwa na TCRA ndio maana amebadirika kimavazi maana mavazi yake sasa ni magauni marefu ila yamebuniwa kwa mitindo tofauti.

Ukiachana na hiyo, Uwoya hivi karibuni amerudi kutoka Dubai ambako alienda kwa ajili ya mapumziko.

Mwanaspoti kama kawaida yake likamnyapianyapia na kupiga naye stori mbili tatu.

Kwanza ni kuhusu kumwagwa na Abdul Chende ‘Dogo Janja’ au Janjaro.

Baada ya kuonekana Dubai akiponda raha bila ya uwepo wa Dogo Janja, watu wakaibua habari ya Uwoya ambaye ni mshindi wa tano wa Miss Tanzania mwaka 2006 ameachika na amepata mwanaume mwingine mwenye pesa aliyempeleka Dubai kula bata.Minong’ono ikadai bwana huyo ndiye anayempa kiburi Uwoya hadi watu kumuona amebadirika kwa mavazi na kutupia vijembe katika ukurasa wake wa Instagram.

Pili, inadaiwa ndoa aliyofunga na Dogo Janja sio ya kweli, bali kuna binti anayeitwa Zaimbaji ‘Zai’ ndiye aliyeolewa na Dogo Janja ila sasa siku ile alishindwa kutimiza jukumu hilo kwa sababu ya ujauzito. Hivyo Uwoya alikwenda kumwakilisha.

Inasemekana lakini Zai ni mwigizaji na watu wengi wanamfahamu kama mdogo wa Uwoya kutokana na kuwa naye karibu, pia kuishi naye nyumba moja.

Tatu, Uwoya amepewa kesi ya kuwaachanisha Aslay na mama wa mtoto wake, Tessy. Baada ya wawili hao kuachana Tessy akawa karibu na Uwoya na kutoka naye sehemu za kujirusha.

Mwanaspoti: Kuna ukweli kuachana na Dogo Janja?

Uwoya: Nasikia hizo habari ila mimi kuachana na Dogo Janja watu watasubiri sana,” anasema mnyange huyo aliyepata umaarufu kwenye filamu ya Oprah akiwa na Vincet Kigosi ‘Ray’ na Steven Kanumba.

Uwoya: Hiyo haitatokea na watasubiri kama embe kwenye mti wa mpapai, ina maana mtu asisafiri peke yake? Au kutoka out peke yake? Ndio waseme nimeachika? Wanataka tugandane Kama Ruba?” Alisema na kuongeza yeye na Dogo Janja hawana mapenzi ya kugandana kila wakati. Kuna muda wanakuwa pamoja na wakati mwingine wanakuwa mbalimbali.

Mwanaspoti: Vipi kuhusu kuwa na bwana mpya?

Uwoya: (kicheko) Dubai mbona kumezua mambo daah! Yaani kwenda Dubai kupumzika ndio nimeenda na bwana mpya? Watanzania tuache kuishi kwa kukariri jamani, ifikie mahala tubadirike, sio kila anayesafiri nje ya nchi basi anasafiri na bwana, wengine tuna hela zetu tunaamua tu kwenda kujipa raha na kubadirisha hali ya hewa. Sina bwana zaidi ya Dogo Janja wangu, maneno tu hayo ya mtandaoni tena kwa wale wanaoishi kwa kukariri.

Mwanaspoti: Lini unatarajia kupata mtoto na Dogo Janja?

Uwoya: Mimi ni mke halali wa Dogo Janja, na mke ni wajibu kumzalia mumewe, hivyo tupo kwenye maandalizi ya kutafuta mtoto ili kuongeza furaha katika ndoa yetu.

Mwanaspoti: Unasemaje kuhusu kumfungia ndoa Zai?

Uwoya: Watu bana, Zai ni mdogo wangu, Dogo Janja ni mume wangu, hakuna kitu kama hicho bana, ifikie mahala watu wakue na wawe bize na maisha yao na sio ya watu.

Mwanaspoti: Unadaiwa kuvunja uhusiano wa Aslay na Tessy?

UWOYA: Kwanza hakuna kitu kinachonikera kama kuhusishwa kwenye inshu ya Aslay na Tessy. Yaani watu wameundaunda maneno ambayo hawayajui kwa undani kati yangu na familia ile.

UWOYA: Labda niwaambie tu, Tessy na Aslay walikuwa majirani zangu na ndio maana niko karibu na Tessy. Hata hivyo, pindi ninapokuwa naye hatuzungumzi kuhusu wanaume wala hizo habari wanazosema.

Uwoya: Tessy ni mtu mzima na anajielewa sana hivi mimi ndio niwe sababu ya wao kuachana? Vitu vingine ni vya kuchekesha sana halafu havina hata pointi. Mimi naangalia maisha yangu, siwezi kufurahi mwenzangu akiharibikiwa.

Advertisement