Twanga Pepeta yapeleka nyimbo mpya Ubungo Maziwa

Muktasari:

Mara ya mwisho Twanga Pepeta kutoa wimbo ambao una maudhui au staili ya bendi hiyo ilikuwa ni mwaka 2012 baada ya kurejea kwa Kalala akitokea Mapacha Watatu na kibao hicho kiliitwa Nyumbani ni Nyumbani.

BENDI ya muziki wa dansi nchini ya The African Stars International ‘Twanga Pepeta’,  leo Ijumaa itatambulisha nyimbo zake nne kwa wadau jijini Dar es Salaam eneo la Ubungo Maziwa kabla ya kutoa albamu yao mpya.
Akizungumza na MCL Digital, Mkurugenzi mpya wa bendi hiyo Luizer Mbutu amesema,Twanga Pepeta kwa mara ya kwanza itapiga nyimbo mpya kwa wakazi wa Ubungo Maziwa ambazo ni 'Penzi Sigara Kali'  uliotungwa na Charles Gabriel 'Chaz Baba', Twanga Mbele wa Kalala Junior, Sukari ya Warembo, Rekebisha ya Msafiri Diof , Sokoine na Povu ya Haji Ramadhani ‘Haji BSS’,.
Luizer amesema nyimbo hizo zimeanza kupigwa kwenye maonyesho mbalimbali ya bendi hiyo, ikiwamo lile la kila Jumamosi.
Mara ya mwisho Twanga Pepeta kutoa wimbo ambao una maudhui au staili ya bendi hiyo ilikuwa ni mwaka 2012 baada ya kurejea kwa Kalala akitokea Mapacha Watatu na kibao hicho kiliitwa Nyumbani ni Nyumbani.
Lakini kabla ya hapo nyimbo ambazo zilikuwa zinaendana ama zina utambulisho wa bendi hiyo ya Twanga Pepeta, ilikuwa kwenye albamu ya Dunia Daraja ambayo ilitungwa na Charles Gabriel ‘Chalz Baba’, ambaye baadaye alitimkia Mashujaa Band mwaka 2012.
Katika albamu hiyo kulikuwa na nyimbo nyingine kali kama Kauli uliyotungwa na Rogart Hega Katapila na Kiapo cha Mapenzi umetungwa na Salehe Kupaza na kufanya vizuri na zaidi ya yote zilikuwa kwenye staili ya bendi hizo ambazo zimezoeleka hata kwa mashabiki wa dansi wakisikia wanajua hao ni Twanga Pepeta.