Twanga Pepeta yaahidi kufunika Wasafi Festival

Muktasari:

Amesema siku hiyo, Mkurugenzi wa bendi hiyo, Luiza Mbutu atacheza nyimbo mfululizo bila ya kupumzika kuwathibitishia mashabiki wake kwamba bado yuko 'fiti' jukwaani.

Bendi ya African Stars Entertainments 'Twanga Pepeta' imeahidi kukonga nyoyo za wapenzi wa muziki watakaojitokeza kushuhudia Tamasha la Wasafi Festival 2019, litakalofanyika Novemba 9, 2019 katika Viwanja vya Posta Kijitonyama, Dar es Salaam, Tanzania.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumanne Novemba 5, 2019, kiongozi wa bendi hiyo, Kalala Junior amesema hivi sasa Twanga Pepeta inafanya mazoezi katika Ukumbi wa Vijana Kinondoni akisema vijana wanaandaa shoo kali itakayokuwa na staili mpya, “kutakuwa na 'Surprise' ya mambo mengi katika safu ya uimbaji, upigaji wa vyombo na wacheza shoo.”

Kalala Junior amesema, mashabiki wa Twanga Pepeta siku hiyo ya tamasha wataiona bendi hiyo kivingine kwani uongozi mpya umebadili mambo mengi.

Amesema kwa kuwa bendi hiyo ina albamu 14 hadi sasa, watatumia fursa hiyo kuimba nyimbo kutoka katika kila moja sambamba na kutambulisha nyimbo zao mpya ambazo alizitaja kuwa ni 'Penzi Sigara Kali' uliotungwa na Charles Gabriel ' Chaz Baba', ‘Twanga Mbele’ alioutunga yeye, ‘Rekebisha’ wa Msafiri Diof na ‘Povu’ wa Haji Ramadhani (Haji BSS). Amesema nyimbo hizo zimeshaanza kuchezwa katika kumbi mbalimbali.

Amesema siku hiyo, Mkurugenzi wa bendi hiyo, Luiza Mbutu atacheza nyimbo mfululizo bila ya kupumzika kuwathibitishia mashabiki wake kwamba bado yuko 'fiti' jukwaani.

Kwa upande wake, amesema ataonyesha ufundi wa kupiga vyombo vya muziki, kama keyboard na gitaa na kuimba. Sambamba nao, amesema mnenguaji mkongwe Supa Nyamwela ataonyesha mitindo mipya itakayoongozwa na mirindimo ya gitaa zito (bass) linalopigwa na Jojoo Jumanne 'Babu'.