Tuwaache kidogo Waandaaji wa Miss Tanzania

Muktasari:

  • Queen Elizabeth ambaye pia ni Miss Kinondoni 2018, Miss Dar Es Salaam 2018 na World Miss University Africa 2017, amewazidi walimbwende wenzake 19 na kuondoka na gari aina ya Terrios Kid. Ni hili gari ndio limesababisha Upupu wa leo.

SHINDANO la kumtafuta mnyange wa Tanzania, Miss Tanzania 2018, limefanyika usiku wa juzi Jumamosi na kushuhudia Queen Elizabeth Makune akitwaa taji hilo.

Queen Elizabeth ambaye pia ni Miss Kinondoni 2018, Miss Dar Es Salaam 2018 na World Miss University Africa 2017, amewazidi walimbwende wenzake 19 na kuondoka na gari aina ya Terrios Kid. Ni hili gari ndio limesababisha Upupu wa leo.

Watu wengi wameonekana kubeza gari hilo kwamba halina hadhi ya kuwa zawadi kwa mshindi wa Miss Tanzania.

Kuna walioenda mbali zaidi na kusema, ni bora mshindi angepewa simu badala ya gari.

Mashindano ya Miss Tanzania, ambayo yalirudi upya 1994 baada ya kufanyika mara moja tu 1967 na kufutwa 1968 na serikali, yametoka mbali sana.

Mwaka 1995, ukazuka ule mgogoro wa mshindi Emily Adolf, aliyeshiriki kutoka Dodoma akiwa mwanafunzi.

Baada ya kushinda, mkuu wake wa shule akamtimua...Waziri wa Elimu enzi hizo, Prof. Philemon Sarungi, akaingilia kati lakini Mkuu wa Shule alisimamia alichokiamini. Waandaaji, kampuni ya Lino International Agencies, walifanya kazi kubwa ‘kuyasimamisha’ mashindano hadi ukafika wakati yakawa juu kupita maelezo.

Kukua kwa thamani ya mashindano kukavutia uwekezaji ambapo pia kuliongeza ukubwa wa zawadi na zaidi ni wadhamini.

Kwa mfano, mwaka 2005, mshindi Nancy Sumari alipewa zawadi ya nyumba ya kisasa kabisa yenye kila kitu ndani (self contained).

Alipoenda ‘huko duniani’ Nancy Sumari akashinda taji la Miss World Afrika na aliporudi nyumbani, alipata mapokezi ya hali ya juu yakiongozwa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete na kufuatiwa na ‘bonge la party’ ndani ya viwanja vya Ikulu. Wakati huo, Miss Tanzania ilikuwa katika ubora wa hali ya juu sana kiasi cha viingilio vya fainali kuwa Shilingi 50,000-100,000 na watu walilipa na kujaza ukumbi.

Lakini kwa miaka ya hivi karibuni, mashindano hayo yaliporomoka kiasi cha kukosa thamani.

Mwaka 2014, serikali kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), iliyafungia mashindano hayo kwa miaka miwili kutokana na ubabaishaji uliokithiri.

Kifungo kilipoisha, mashindano yakarudi mwaka 2017 lakini hayakuwa na mvuto kabisa.

Mapema mwaka 2018, Lino International Agencies, chini ya ‘anko’ Hashim Lundenga, ikaachana na mashindano hayo na kumkabidhi mshindi wa Miss Tanzania 1998, Basila Mwanukuzi ili ayafufue upya.

Kwa sasa, Mwanukuzi anahangaika kurudisha heshima ya mashindano hayo ambayo wakati wa ubora wake, wadhamini walikuwa wakishindana kujihusisha nayo.

Miss Tanzania kwa sasa haina mvuto, haina udhamini wala haina muitikio wa watazamaji ukumbini.

Ni vigumu sana kwa waandaaji kuweza kutoa zawadi kama zilizotolewa katikati ya miaka ya 2000 wakati wa kilele cha ubora cha mashindano hayo. Katika kipindi hiki cha kuyasimamisha mashindano, inabidi watu wengi hasa wadau wa urembo, wajitoe bila kuangalia maslahi, kwa faida ya tasnia yenyewe.

Wadau hapo ni pamoja na walimbwende wenyewe, hakuna mtu kutoka nje ya tasnia husika, atakayekuja kuyafanya mashindano hayo yawe makubwa. Naamini hata Basila mwenyewe wakati akishinda mwaka 1998, hakupata zawadi ya maana zaidi ya kile kichwa cha habari cha, “Yes Mwanukuzi, tumekunukuz kwa mavituz” kwenye moja ya magazeti ya udaku ya wakati ule.

Wakati Basila anahangaika ‘kuinua upya brand’ ya Miss Tanzania, sisi tuliobaki tunatakiwa kumuunga mkono na kumtia moyo badala ya kumbomoa na kumkatisha tamaa.

Angalau wao wamejitahidi kutoa hiyo zawadi inayopondwa na kubezwa mitandaoni.

Kwenye soka, Shirikisho la mchezo huo (TFF) limeshindwa kutoa zawadi kwa washindi wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports, Mtibwa Sugar, tangu Mei 2, mwaka huu.

Kombe la Shirikisho la Azam Sports lina mdhamini kama jina lake linavyojieleza... mdhamini ambaye hutoa pesa na zawadi zote mapema kabisa, lakini hadi sasa Mtibwa hawajapewa stahiki yake.

Mtibwa Sugar hao hao, timu yao ya vijana chini ya miaka 20, ilishinda ubingwa wa Ligi Kuu kwa umri wao mwezi Julai mwaka huu, nao hadi leo hawajapewa zawadi zao. Mashindano hayo pia yana mdhamini mkubwa kabisa.

Sasa kama mashindano yenye wadhamini kama hayo, hakuna zawadi hadi sasa...vipi kuhusu mtoto yatima Miss Tanzania?

Tuwaache kidogo jamani nao wapumue!