Tommy Flavour: Kiba hafi njaa hata asipofanya muziki

Sunday October 18 2020

 

By KELVIN KAGAMBO

Nadharia nyingi uibuka linapokuja suala la kuwashindanisha mafahari wawili wa Bongofleva nchini, Alikiba na Diamond. Moja ya nadharia hizo ni ile inayosemwa kuwa Alikiba ni mwanamuziki wakati Diamond ni mfanyabiashara.

Huku nadharia hiyo ikibebwa na data za kwamba Diamond anamiliki biashara nyingi kubwa zinazofahamika kuliko Alikiba, vitu kama vile kituo cha redio na televisheni, lebo ya muziki, bidhaa ya manukato na zaidi.

Mwandishi wetu alipata nafasi kuzungumza na moja ya wasanii wanaofanya kazi chini ya lebo ya Alikiba, Kings Music, Tommy Flavour na kumuuliza mtazamo wake kuhusu nadharia hiyo, Tommy amejibu:

“Ni theory za mitandaoni tu, hazina ukweli. Na zinasemwa kwa sababu watu wanajaji kupitia social media. Mimi Kiba ni braza wangu na najua ni mfanyabiashara mzuri, ana biashara ambazo hata leo akiacha muziki ataendelea kuishi bila njaa.” ameeleza Tommy ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wake wa The One.

Tommy alibanwa zaidi na kuombwa ataje biashara anazomiliki mkali wa masauti Alikiba, hata hivyo alichomoa.

“Kama mmliki hazizungumzii Instagram, mimi pia sioni sababu ya kuzisema hapa. Ninachojua ni hiyo theory haina ukweli. Alikiba ni mzuri pande zote, muziki na biashara.” amesema.

Tommy ni msanii aliyesajiliwa na lebo ya Kings Music Machi 2018 kama msanii wa sita wa lebo hiyo. Kisha akiwa Kings akaachia ngoma yake ya kwanza ambayo alimshirikisha Alikiba, Omukwano, wimbo ambao ulikuwa hit mtaani.

Advertisement