Tamasha la muziki la Marafiki kukutanisha wadau wa Muziki

VIKUNDI 13 vya wanamuziki wa Tanzania na mmoja wa Kenya vitatumbuiza kwenye tamasha la kwanza la muziki liitwalo Marafiki litakalofanyika kwa siku tatu sehemu mbili tofauti ikiwemo Dar es Salaam na Bagamoyo.

 

Mkurugenzi wa Tamasha hilo Isack Abeneko amesema tamasha hilo litafanyika kuanzaio keshokutwa Alhamisi, Oktoba 8 hadi 10 mwaka huu.

 

Tamasha hilo lenye kauli mbiu Utamaduni ni ngao ya Taifa litafanyika Slow Leopord Masaki Oktoba 8 na 9 na Oktoba 10 tamasha litakua Bagamoyo Firefly kwa kiingilio  cha Sh10,000 ambapo tamasha litaanza saa 1 jioni mpaka saa sita usiku kila siku.

 

 “Huu ni msimu wa kwanza wa Tamasha linalolenga kuleta fursa zaidi kwenye shughuli za kimaendeleo ya jamii kupitia jukwaa la muziki mubashara.Wazo la tamasha hili lilizaliwa kutokana na tukio la Marafiki Night Live ambalo hufanyika mara moja kwa mwezi kuazia Oktoba 2018.

 

"Tukio hili huleta marafiki na wadau wa muziki kufurahia muziki kwa pamoja, kupitia jukwaa la Marafiki Night Live tuliona kuna umuhimu wa kuanzisha tamasha hili ambalo litatoa fursa zaidi kwa wadau wa muziki kupata nafasi ya kuonyesha kazi zao na wengine kupata nafasi ya kujifunza kutoka kwa wenzao,”amesema Abeneko.

 

Abeneko amewataja wasanii watakaotumbuiza kuwa ni Wamwiduka Band , Ze Spirits Band, DDC Mlimani Park – Sikinde, Abeneko & Positive mind, Rich Lumambo, Malfred, Siti & The band (Zanzibar), Afro Simba Band (Kenya), Upendo Manase, Shabo Makota, Msafiri Zawose, Baba Kash na Tamimu.

 

“Utofauti wa tamasha la Marafiki na matamasha mengine ni namna tamasha lilivyoanza kwa kuunganishwa na urafiki ndani ya tasnia ya muziki na sasa tamasha linaanza kwa kuleta pamoja marafiki wa muziki na wanamuziki pamoja waungane  kupitia muziki na kupata fursa ya kushiriki tamaduni mbalimbali kupitia muziki,” amesema Abeneko.

 

Shaban Mugado Meneja wa Tamasha amesema, ASEDEVA kwa kushirikiana na Weka Music Records wameandaa tamasha hilo ambalo mbali na burudani ya muziki tamasha litaambatana na warsha zitakazosaidia wadau wa muziki kukuza uelewa wao kupitia mada zitakazotolewa wakati wa tamasha hilo la siku tatu.

 

“Tamasha litakua na mada mbalimbali kwenye warsha ambazo zitawasaidia wasanii kuongeza thamani kwenye kazi zao za kimuziki ili kukuza sanaa ya muziki pamoja na kuwajengea uwezo. Tutajadili biashara ya muziki, usimamizi binafsi wa mwanamuziki na hata baada ya kupata meneja, namna ya kupata nafasi za maoneysho ya Kimataifa na Uhandisi wa sauti.

 

"Oktoba 8 na 9 kuanzia saa 4:00 asubuhi mpaka saa 7:30 mchana warsha zitafanyika Nafasi Art Space Mikocheni,” amesema Mugado.

 

Mugado amewashukuru wadhamini wa Tamasha ambao ni Goethe-Institut Tanzania, Firefly Bagamoyo, The Slow Leopard Bar & Restaurant, Jameson, Busara promotion, Boresha Radio, Acto Light, Nafasi Art Space, EM media, Ruka Company, Basata na Eyecue Media Solution.