Tamasha la Sauti za Busara labeba ajenda mpya

Muktasari:

  • Baadhi ya wasanii watakaounga mkono jitihada za kusambaza ujumbe wa kukabiliana na rushwa ni pamoja na Faith Mussa (Malawi), Fadhilee Itulya (Kenya), Fid Q (Tanzania), BCUC (Afrika Kusini) na wengineo watakaokuwa wakitumbuiza katika tamasha.

Maandalizi ya tamasha la 16 la Sauti za Busara yanaendelea huku wahudhuriaji kutoka ndani na wale wageni wa kimataifa wanajiandaa kwenda Zanzibar kushuhudia muziki wa Kiafrika unaopigwa jukwaani moja kwa moja.

Busara Promotions limethibitisha kuwa mpangilio wa tamasha hilo lililojizolea heshima kubwa miongoni mwa watu upo vizuri kwani lilianza rasmi siku ya Jumanne, Februari 7 na linaendelea.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Yusuf Mahmoud kaulimbiu ya tamasha la mwaka huu inalenga kupambana na rushwa kwa kuwa wanaamini wasanii wanaweza kutumia sauti zao kukabiliana na tatizo hilo wakati wanasheherekea utajiri na mkusanyiko wa tamaduni mbalimbali za muziki wa Afrika.

“Katika kuunga mkono wasanii wanaotumia muziki kusimamia amani, umoja, haki za binadamu na uhuru wa kujieleza, ujumbe wenye nguvu ambao unaonekana katika tamasha la mwaka huu ni (“Potezea Rushwa, Sio Dili!),” alisema Mahmoud.

Aliongeza kuwa, “Rushwa ni janga linalotafuna na linalomomonyoa maadili ya jamii zetu barani Afrika na nje ya Afrika. Kibaya zaidi imefikia hatua kuwa hata baadhi ya watu wamekuwa wakichukulia ni jambo la kawaida.

Hata hivyo, tamasha moja pekee haliwezi kubadili jamii yote kikamilifu, hivyo, tunashirikiana pamoja na washirika wa ndani na wa kimataifa kuendeleza majadiliano au mazungumzo, kubadili mitazamo na kuchochea hatua mbalimbali kwa ajili ya uongozi bora,” anasema Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara.

Baadhi ya wasanii watakaounga mkono jitihada za kusambaza ujumbe wa kukabiliana na rushwa ni pamoja na Faith Mussa (Malawi), Fadhilee Itulya (Kenya), Fid Q (Tanzania), BCUC (Afrika Kusini) na wengineo watakaokuwa wakitumbuiza katika tamasha.

Tamasha la Sauti za Busara la mwaka 2019 linadhaminiwa na Ubalozi wa Norway, Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na Zambia, Umoja wa Ulaya, Africalia, Ubalozi wa Ufaransa, Ubalozi wa Ujerumani, Pro Helvetia, TV- E, E-FM, Zanlink, Mozeti, Shirika la Ndege la Ethiopia, African Movie Channel, Zanzibar Media Corporation na wengine.