Tamasha la Pasaka kulindima Dar es Salaam

Muktasari:

 

  • Maudhui ya msingi ya tamasha hilo, ni kueneza ujumbe wa Neno la Mungu kupitia waimbaji, kukuza muziki wa injili ili kutoa ajira kwa vijana wenye vipaji vya kuimba.

Dar es Salaam. Tamasha la Pasaka litafanyika Jijini Dar es Salaam baada ya kushindwa kufanyika kwa miaka miwili halikuweza kufanyika katika jiji la Dar es Salaam kutokana na sababu maalumu zilizowahi kuelezwa na waratibu wa tukio hilo la kimataifa.

Waandaji wa tamasha hilo kongwe kampuni ya Msama Promotions Ltd imesema safari hii likitarajiwa kuanzia jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama amesema baada ya tafakuri ya kina pia kwa kuzingatia maoni ya wadau wa muziki wa injili, wameamua kurejesha tukio hilo jijini humo.

“Kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo tamasha la Pasaka lilikuwa likifanyika mikoani tu, lakini kwa mwaka huu litafanyika pia katika jiji hilo kwa sababu vilio vya wadau wa muziki wa injili ni vikubwa,”alisema Msama.

Alisema mbali ya malengo ya msingi ya kueneza ujumbe wa Neno la Mungu na sehemu ya mapato kusaidia makundi maalumu, safari hii tamasha hilo litatumika pia kuhimiza hali ya amani chini ya kaulimbinu isemayo ‘Upendo, haki na Amani ndio msingi wa amani.’

Msama alisema tofauti na miaka mingi, safari hii wamejiandaa kuhakikisha linakuwa la kimataifa zaidi ikiwemo kuwaleta waimbaji mahiri wa kutoka nje watakaoshirikiana na wengine wa Tanzania.

Mbali ya Dar es Salaam, Msama alisema tamasha hilo litafanyika pia katika mikoa mingine 10 ambayo itajulikana baadaye kwa kuzingatia vigezo stahiki vilivyowekwa na kamati ya maandalizi.

Chini ya maudhui ya msingi ya tamasha hilo, ni kueneza ujumbe wa Neno la Mungu kupitia waimbaji, kukuza muziki wa injili ili kutoa ajira kwa vijana wenye vipaji vya kuimba na kumiliki jukwaa na wauzaji wa kazi za kimuziki.

Kupitia tamasha hilo waimbaji mbalimbali wa kimataifa kama Solly Mahlangu, Sipho Makabane na Rabeca Malope wa Afrika Kusini wamefanikiwa kutumbuiza nchini.

Waimbaji wengine ambao wamekuwa wakija kupamba tamasha hilo karibia kila linapofanyika, ni kutoka Kenya, Rwanda, DR Congo, Zambia pamoja na Uingereza.