Tamasha Dk Tulia lazidi kushika kasi

Muktasari:

  • Tamasha hilo litafanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 20 Rungwe mkoani Mbeya na litashirikisha vikundi vya ngoma 108 na zaidi ya watu 2,000 wanatarajiwa kushiriki.

Dar es Salaam. Msimu mpya wa Tamasha la Ngoma za Jadi (Tulia Traditional Dances Festival) umezinduliwa na mratibu wa tamasha hilo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amesema litashirikisha vikundi vya ngoma mikoa yote nchini.

Tamasha hilo litafanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 20 Rungwe mkoani Mbeya na litashirikisha vikundi vya ngoma 108 na zaidi ya watu 2,000 wanatarajiwa kushiriki.

“Tamasha letu la ngoma za jadi linazidi kutanua wigo kila mwaka, tulipoanza tulikuwa na vikundi 63 kutoka mikoa miwili, mwaka uliofuatia (2017) vikundi 89 kutoka mikoa 17, lakini mwaka huu mikoa yote ya Tanzania Bara na visiwani (Zanzibar) itashiriki,” alisema Dk Tulia.

Alisema zawadi kwa washindi zimeboreshwa ambapo mwaka huu watatoa pikipiki kwa vikundi vitakavyoshinda na fedha taslimu na ofa ya masomo Chuo cha Sanaa Bagamoyo (Tasuba).

“Tunatarajia litakuwa tamasha kubwa la kipekee ambalo litatangaza utamaduni wetu nje ya Tanzania na kuvutia pia watalii kuja nchini kushuhudia,” alisema Dk Tulia.

Naibu Spika alisema vikundi vilivyoshinda tamasha la mwaka jana vimekata tiketi ya kushiriki tamasha la msimu huu.

Alisema upande wa Mbeya vikundi vitakavyoshiriki vitaanza kuchuana katika ngazi ya Kijiji hadi Halmashauri na washindi watashiriki tamasha hilo kitaifa.

“Utaratibu huu unaofanyika mkoani Mbeya ndiyo tunafikiria kwa baadaye ufanyike na mikoa mingine pia, lakini kwa kuanza tumeanzia Mbeya lakini tunafikiria mchakato huo uende kwenye mikoa mingine lengo ni kupanua wigo wa kupata idadi kubwa ya washiriki,” alisema Dk Tulia.