Takes Zenji to the World

Muktasari:

Akizungumza mara baada ya kumaliza kutoa burudani, Lulu anayetamba na albamu ya ‘Thembassa’, alisema hashangazwi na hali hiyo kwani amekuwa akifanya matamasha makubwa ya utamaduni kwenye mataifa mbalimbali ikiwemo Canada, Norway, Uswisi na China.

KILA aliyetia timu kwenye tamasha la Sauti za Busara huko Zanzibar, basi ameondoka huku moyo wake ukiwa umesuuzika kabisa. Kila burudani ilikuwepo na mashabiki muda wote walikuwa na mzuka mwingi kinoma. Kwa mwaka huu, tamasha hilo lilikuwa na vionjo mbalimbali hasa ngoma za kitamaduni ambazo zilikonga mioyo ya mashabiki.

Licha ya takriban asilimia 70 ya mashabiki waliohudhuria kwenye tamasha hilo kuwa ni wageni, lakini walionekana kupagawa zaidi na wasanii huku msanii wa ngoma za kitamaduni kutoka Kenya, Lulu Abdallah akiwa kivutio.

Kilichowavutia mashabiki kwa Lulu ni uwezo wake wa kucharaza gitaa na kushambulia jukwaa kwa wakati mmoja.

Akizungumza mara baada ya kumaliza kutoa burudani, Lulu anayetamba na albamu ya ‘Thembassa’, alisema hashangazwi na hali hiyo kwani amekuwa akifanya matamasha makubwa ya utamaduni kwenye mataifa mbalimbali ikiwemo Canada, Norway, Uswisi na China.

“Hii inadhihirisha kwamba maneno ninayoyasema kila siku yana ukweli ndani yake, vyombo vya habari havithamini muziki wa asili, lakini tunatambulika sana nje, hii ndiyo maana ya kile kilichotokea hapa,” alisema Lulu.

Guiss Guiss Bou Bess kutoka Senegal , FRA wa Ghana, Thais Diarra kutoka Mali, TaraJazz wa Zanzibar na Siti & the Band kutoka Zanzibar pia walionyesha uwezo wa hali ya juu.

Mwanaspoti ambalo liliweka kambi kwenye tamasha hilo tangu siku ya kwanza likikupa burudani zote, siku ya pili ya tamasha mwanamuziki Apio Moro kutoka Uganda aliwafanya mashabiki waendelee kuufurahia muziki bila kuhofia mvua kama ingewanyeshea. Apio ni mwanamuziki wa kike anayeimba miondoko ya Afro-Soul.

Akizungumza mara baada ya kutumbuiza, Apio alisema amepata uzoefu wa kuimba kupitia mfumo wa maisha na amewawezesha watu wengi kujua jinsi gani wanaweza kutumia muziki kueleza maisha yao.

“Mimi natokea Tororo, Uganda ya Mashariki, ni mwimbaji na mwandishi wa nyimbo, hivyo kupitia mfumo wa maisha yangu nimewezesha watu wengi kujua jinsi gani wanaweza kutumia muziki kueleza maisha yao,” anasema.

“Huwa simuahidi mtu au watu kuteka hisia zao au mihemko, bali nitakubeba taratibu na kumaliza yote na kukuacha umeridhika kumuziki.”

Katika tamasha hilo, kundi la Swahili Encounters liliwakusanya wasanii kutoka Zanzibar, Moroco, Ghana, Uingereza, Tanzania, Algeria na kuimba wimbo wa pamoja unaohamasisha kaulimbiu ya Tamasha la Sauti za Busara, na mwaka huu ilikuwa ni ‘Paza sauti, pinga unyanyasaji wa kijinsia’.

Kundi hilo lilinogesha kinoma katika tamasha hilo siku ya Ijumaa kwa ujumbe huo.

Mwanamuziki Oumar kutoka Mali alifungua shoo siku hiyo iliyokaribishwa na mshehereshaji Masanja Mkandamiza ambaye pia ni msanii - mchekeshaji.

Wasanii wengine walioonyesha mambo yao kwenye tamasha hilo katika mji wa Ngome Kongwe ni Pigment wa Reunion, Nadi Ikhwan Safaa kutoka Zanzibar, Kaloubadya wa Reunion na Mamy Kanoute kutoka Senegal.

Siku ya tatu wanamuziki wa Tanzania Wakazi, The Mafiki na Mopao Swahili Jazz walipanda jukwaani kutoa shoo ya nguvu ambapo ukumbi wa Ngome Kongwe ulifuruka zaidi

Nyota hao walizungumzia kuhusiana na ujazo wa watu tamashani ambapo walisema ni zaidi ya tamasha kutokana na ‘mafuriko’ ya mashabiki huku wakisisitiza kuwa kuwa hali ikiendelea hivyo mwakani ufanyike utaratibu wa kuongezwa sehemu ya ukumbi au eneo husika.

Wasanii wengine waliotumbuiza Jumamosi ni Ambasa Mandela & the Last Tribe wa Kenya, Mamy Kanout’e kutoka Senegal, Mannyok (Mauritius), Mapanya Band (Zanzibar), Mehdi Laifaoui Trab Project (Algeria), Mehdi Qamoum (Morocco), Onipa ( Ghana) pamoja na Siti & the Band kutoka Zanzibar.

Siku ya nne kundi la muziki wa asili la Mopao Swahili Jazz kutoka Tanzania lilitia fora kwa kuimba nyimbo zenye mafunzo na zinazochezeka.

Licha ya uwepo wa Onipa kutoka Ghana, walicheza muziki wa asili na Kiarabu huku wakichanganya maneno ya Kiswahili vikinogeshwa na sauti bora zilizopangiliwa.

Tamasha la Sauti za Busara lilimalizika Februari 16 katika viwanja vya Ngome Kongwe mjini Zanzibar na mwanamuziki Evon kutoka Uganda alikonga mioyo ya mashabiki.

Wasanii wengine waliotumbuiza katika hitimisho la tamasha hilo ni pamoja na FRA wa Ghana, Ison Mistari a.k.a Zenji Boy, Mehdi Laifaoui Trab Project kutoka Algeria na Oumar Kont’e wa Mali.

Changamoto

Wakati tukizungumzia mazuri ya tamasha hilo, miaka 15 nyuma, mwaka 2020 umekuwa wenye changamoto kutokana na matatizo kadhaa ambayo yalilalamikiwa na baadhi ya wanamuziki kutoka nje.

Hata hivyo, matatizo mengine yalikuwa ni ya kiufundi sambamba vipaza sauti kukata baadhi ya wanamuziki walipopanda jukwaani.

Baadhi ya wanamuziki walilalamikia suala la kutunza muda na kuna wakati ilikuwa ikichukua zaidi ya nusu saa kuandaa jukwaa kwa ajili ya mwanamuziki mwingine kutumbuiza.

Hilo ni tamasha la 17 la Sauti za Busara ambalo lilianza Februari 13 na kumalizika Februari 16, ambapo siku ya ufunguzi kabla ya kuingia ukumbi wa Ngome Kongwe vikundi zaidi ya 16 vya Zanzibar vilionyesha uwezo wa sanaa mbalimbali ikiwemo ya ngoma, sarakasi na muziki katika maandamano maalumu.

Vikundi hivyo viliongoza maandamano ya umbali wa kilomita 1.6 kutoka eneo la Mapinduzi Square, ambapo njiani hadi kufika viunga vya bustani ya Forodhani (Ngome Kongwe) vilionyesha uwezo wa sanaa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Busara Promotion, Mohamed Simai ambaye pia ni naibu waziri wa Elimu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alilifunga kwa kusema ilikuwa ni furaha kuona wazo la watu saba (waanzilishi) limekuwa na faida kwa wengi.

“Tulianzisha tamasha hili watu saba, leo hii limekuwa na mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi, jamii inafaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na tamasha hili,” alisema Simai.

Aliongeza kuwa katika timu ya waasisi wa tamasha hilo miongoni mwao alikuwapo Ruge Mutahaba, ambaye ametangulia mbele za haki pamoja na Mzee Makame Faki Makame.

Tamasha hilo hufanyika kila mwaka katika eneo la Mji Mkongwe mjini Zanzibar.