Stara Thomas awalipua wasanii wanaotumia dawa za kulevya

Wednesday February 13 2019

 

By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, Stara Thomas amesema wasanii wamekuwa wakidanganyana kuwa bila ya kutumia dawa za kulevya huwezi kuwa na 'swaga'.

Stara ameyasema hayo leo Jumatano kwenye kongamano kuhusu tatizo la dawa za kulevya kwa wasanii lililoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo linafanyika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere.

Stara alisema kauli hizo kwamba bila msanii kutumia dawa za kulevya huwezi kuwa na swaga zimewapoteza wengi ambao wengine wamejikuta wakiingia katika mtego huo.

 "Tuna ushuhuda wengi tumepoteza kwa kutumia dawa za kulevya aidha kwa kujua au kufuata mkumbo kama hivyo kuambiwa ili uwe na swaga yapaswa kutumia.

 " Hata hivyo hatupaswi kuwatenga pamoja na wao kuingia humo isipokuwa tusichoke kuwapa elimu ya mara kwa mara na kwa wale wanatarajia kuingia huko, wasithubutu kwani watapoteza ndoto zao na kuziacha familia zao katika huzuni,"amesema msanii huyo ambaye aliwahi kutesa na wimbo wa 'Nashindwa na ile wa ' Mimi na Wewe'.

Alibainisha kwamba changamoto kubwa walionayo ni kwamba kazi zao wengi wanazifanya katika maeneo yaliyozungukwa na vilevi, hivyo msanii asipokuwa makini ni rahisi kuingia kwenye utumiaji dawa za kulevya.

Kongamano hilo limehudhuriwa na wasanii was gani mbalimbali wakiwemo wa filamu, muziki, sanaa za maonyesho, ngoma, sarakasi pamoja na washehereshaji huku kaulimbiu ikiwa ni 'Usanii bila kutumia dawa za kulevya inawezekana, chukua hatua'

Advertisement