Skide, Fid Q kunogesha Sauti za Busara 2019

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tamasha la Busara, Yusuf Mahmoud, kuna mambo mengi ya kutazamiwa katika tamasha la mwaka huu.

Zanzibar na Afrika Mashariki wanajiandaa kufanya Tamasha la Sauti za Busara la mwaka 2019 likiwa na azma ya kuupeleka muziki wa kipekee wa Kiafrika unaopigwa mubashara (live) kwenda kwenye hatua nyingine kitaifa na kimataifa.

Tamasha hilo linalofuatiliwa ulimwenguni kote linatarajiwa kuanza rasmi Februari 7, Old Fort likiwa na maonyesho ya kusisimua 46 kutoka kwa zaidi ya wasanii 400 katika majukwaa matatu tofauti kwa siku nne yaani mchana na usiku.Makundi mengi yatakuwa yanatumbuiza katika jukwaa hili la Sauti za Busara la aina yake kwa mara ya kwanza.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tamasha la Busara, Yusuf Mahmoud, kuna mambo mengi ya kutazamiwa katika tamasha la mwaka huu.

“Kwa miaka kadhaa sasa, watazamaji wamekuwa wakitarajia vitu vya kipekee na vipya kila wakati. Tunaamini orodha ya mwaka huu, pia ni bora kuwahi kutokea, kwani tunaendelea kuonyesha muziki halisia wa Kiafrika wenye utambulisho,” anasema Mahmoud.

Wakati huo huo, Meneja wa Tamasha la Sauti za Busara, Journey Ramadhan anasema kutakuwa na mambo mapya na sauti mbalimbali za kuvutia kutoka Tanzania ikiwemo  Wamwiduka Band na Skide, wasanii wa muziki aina ya “Singeli” ambao wataudhihirishia ulimwengu utajiri wa muziki huo wa kizazi kipya ambao asili yake ni Tanzania.

“Ni imani yangu kuwa baada ya kuisha kwa burudani hizo katika Tamasha mambo hayatabaki kama yalivyokuwa, kama ambavyo historia imekuwa ikijirudia kwa makundi mengine yaliyowahi kutumbuiza katika tamasha la Sauti za Busara katika miaka iliyopita, makundi kama vile Sarabi, Jagwa Music, Tausi Women’s Taarab na mengine,” aliongeza Journey Ramadhan.

Orodha ya wasanii watakaokuwepo katika tamasha la Sauti za Busara la mwaka 2019 ni pamoja na Mokoomba (Zimbabwe), Fid Q ( Tanzania), BCUC (Afrika Kusini), Afrigo Band (Uganda),Fadhilee Itulya (Kenya), Mkubwa na Wanawe Crew (Tanzania), SKide(Tanzania), Damian Soul (Tanzania),Jackie Akello (Uganda), Faith Mussa (Malawi), Asia Madani (Sudan/Misri), M’ToroChamou (Mayotte), HobaHoba Spirit (Morocco), Shamsi Music (Kenya), Sofaz (Reunion), Dago Roots (Reunion), Lydol (Cameroun), Stone Town Rockerz (Zanzibar), Ithrene (Algeria), Ifrikya Spirit (Algeria), Trio Kazanchis + 2 (Ethiopia/Switzerland), Rajab Suleiman & Kithara (Zanzibar) na wengine wengi.

Tamasha la mwaka 2019 litakuwa ni jukwaa kwa wasanii na hadhira kutoka sehemu mbalimbali duniani kuungana kwa pamoja na kusema “hapana” dhidi ya vitendo vya rushwa, wakishinikiza viongozi kutoka katika kila sekta kutimiza majukumu yao ya kila siku pasi na mianya ya vitendo vya rushwa.

Tamasha la Sauti za Busara linadhaminiwa na Ubalozi wa Norway, Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na Zambia, Umoja wa Ulaya, Africalia, Ubalozi wa Ufaransa, Ubalozi wa Ujerumani, Pro Helvetia, Zanlink, Mozeti, Shirika la Ndege la Ethiopia, African Movie Channel, Zanzibar Media Corporation na wengine wengi.