Shilole, Faraja Kotta wafunika kwa Malkia

Muktasari:

  • Katika kipengele cha mfanyabiashara wa chakula, msanii wa filamu na Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ alinyakua tuzo hiyo.

TASNIA ya burudani imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika jamii na hilo limeonekana hadi kwenye Tuzo za Malkia wa Nguvu, ambapo wasanii, wanamitindo na warembo wamezibeba za kutosha tu.

Katika tuzo hizo ambazo kilele chake kilifikia juzi Jumamosi, Miss Tanzania 2004, Faraja Nyalandu, Shilole, Miriam Odemba, Asha Baraka na Leah Mwendamseke walishinda tofauti na huko nyuma wakati zinaanzishwa.

Tuzo hizo ambazo zinaingia msimu wake wa nne zikiwa chini ya Kampuni ya Clouds Media, zinalenga kutambua mchango na kazi zilizofanywa na wanawake katika jamii.

Katika kipengele cha mfanyabiashara wa chakula, msanii wa filamu na Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ alinyakua tuzo hiyo.

Ushindi huo unakuja kutokana na kuanzisha mgahawa wake Shishi Food, ambapo mbali na kutoa huduma ya chakula, kwa namna fulani amekuwa akihamasisha wanawake kujikita kwenye biashara hiyo huku akitoa ushuhuda kwamba, alianza kama mama ntilie.

Akizungumza wakati wa kupokea tuzo hiyo, Shilole alisema alishawishi wanawake wengi wakiwamo wasanii kufanya biashara hiyo na anashukuru leo wengi wameona fursa hiyo na sasa amebeba tuzo.

Kwa upande wake Faraja, ambaye ni mke wa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, yeye amebeba tuzo ya Mwanamke mwenye ushawishi, akiwa ndiye bosi wa Taasisi ya Shule Direct.

Mbali na Faraja, wengine ni Leah Mwendamseke maarufu kama Lamata, ambaye ni muongozaji na mtunzi wa tamthiliya ya ‘Kapuni’, akibeba tuzo kupitia kipengele cha Mwanamke wa Burudani. Tuzo kama hiyo pia imekwenda kwa Mkurugenzi wa African Stars, Twanga Pepeta, Asha Baraka.