Sekidobwa unarudisha zama za Mwinjuma

Muktasari:

  • Abdulfareed ni mtunzi na mdau mkubwa wa muziki wa dansi zaidi ya miaka 20, huwa anatunga nyimbo kupitia kundi lake linaloitwa Phanton Musica, amesema jina la Wimbo wa Sekidobwa ni jina halisi la kabila la Wabondei.

“UMEKUJA kuwa sinichi uzeeniii, nilitarajia mambo hayo wafanye wajukuu zako sio wewe Sekidobwaaaa, aaah, mtaani umedhalilika kila mtu anakuita jina lakee shilawadu wewe Mkosa hekima wewe, Bwege Nazi weeee umekuwa kama mkosa radhi sekidobwa, kila jambo lako halitengemaiii.”

Hayo ni baadhi ya maneno aliyoyaimba, Muumin Mwinjuma kwenye wimbo mpya wa ‘Sekidobwa.

Wimbo huo umetungwa na Abdulfareed Hussein, na kuimbwa na wanamuziki wanne akiwemo Muumini wengine ni Edo Sanga, Rijo Voice, Fadhili Mnara, huku wapiga vyombo ni Hosea Mgohachi ‘Bass’, Kang’ombe Mashine na Rashid Pembe.

Kwa ukweli Muumin akitendea haki kipande alichopewa kuimba na kusababisha wimbo huo kupenda na wadau wa muziki wa dansi nchini.

Abdulfareed ni mtunzi na mdau mkubwa wa muziki wa dansi zaidi ya miaka 20, huwa anatunga nyimbo kupitia kundi lake linaloitwa Phanton Musica, amesema jina la Wimbo wa Sekidobwa ni jina halisi la kabila la Wabondei.

Abdulfarred mara kibao amekua akiwashika vilivyo mashabiki wake kwa jinsi ya utungaji wake kwani kama uliwahi kuusikia Wimbo wa Sononeko la Huba ulioimbwa na Edo Sanga, Rijo Voice na Fadhili Mnara huku wapiga vyombo wakiwa ni Zahoro Bangwe, Fadhili Mnara, Saddy Ally na Davido Bass, basi jua nyuma wa wimbo huo alikuwa Abdulfareed Hussein.

Fareed anasema kundi lake siyo bendi rasmi, bali huwa linawakutanisha wanamuziki wanaoendelea kuzitumikia bendi zao hasa Msongo Ngoma na wanamuziki wengine wenye vipaji.

“Lengo ni kuwapa wigo mpana wanamuziki waonyeshe uwezo wao ukizingatia bendi nyingi siku hizi hazitoi kazi mpya wala albamu na kuwainua vijana chipukizi wenye vipaji vya mziki huu.”