Seba wa Harmonize na Tale wa Diamond yupi meneja mkali ?

KAMA vipi leo shoo iende kwa mameneja tujue nani mkali. Sebastian Ndege wa Harmonize au Babu Tale, Sallam na Said Fella wa Diamond Platnumz? Mada hii haijapita salama bila Luqman Maloto na Dk Levy kusemeana maneno ‘mbofumbofu’. Je, Samatta anakosa magoli au anajikosesha?

LUQMAN: Katika kambi yenu ya Konde Gang mmeshafanya upelelezi kugundua nani mhusika halisi wa figisu za kulichomoa Uno la Harmonize YouTube? Sio wale jamaa walipenyeza rupia kusababisha uzia?

DK LEVY: Mbona Uno imerudishwa tena YouTube? Ila ya Baba Lao ndo imeanza kupigwa zengwe kuwa WCB wameiga. Ndugu yangu unapitwa na wakati kama upepo wa kisulisuli. Jiongeze Konde Gang haina kufeli.

LUQMAN: Elewa swali, Uno limerudishwa sawa, na aliyelitowesha anafahamika, swali yule jamaa ni yeye au figisu za mtalaka? Usijifanye hujui maswali. Halafu Baba Lao sio issue, mbona inafahamika kuwa Diamond alisampo Soapy wa Naira Marley? Tena kwa makubaliano? Hajaiba. Wewe ndio wa kukuuliza upo wapi? Umejifungia kwenye Lipuli ya Chifu ya Mkwawa nini? Huoneshi kama tupo wote mjini hapa.

DK LEVY: Najua umetumwa na mabeberu wa WCB. Siwezi kukushangaa ninachofahamu ni kwamba UNO bado linarindima YouTube kama kawa. Ninyi vibaraka wa mabeberu wa WCB hamtusumbui vichwa vyetu Team Konde Gang. Kama Mondi amefanya kwa makubaliano tambua kuwa UNO pia ipo YouTube tena kwa makubaliano pia. Konde Boy anawapasua vichwa sana. Sajili wahuni wenu wengine. Kwani bila Konde Boy hiyo WCB inakufa?

LUQMAN: WCB haiwezi kufa wewe, acha kuota. Una Babu Tale na Said Fella itakufa vipi? Harmonize amechukuliwa na Sebastian Ndege, mtu ambaye hana historia ya kumsimamia mwanamuziki hata mmoja. Tale Tip Top, Madee, MB Dog, Tundaman, Keisha, Kassim Mganga, Z-Anto, Pingu na Desso ongeza wengine. Fella hesabu TMK Wanaume Family, Nature, Chegge, Temba, KR, YP, Y-Dash, Luteni Karama, niendeleee? Sasa huyo Seba atampeleka wapi Harmonize? Si ndio maana Konde Boy katoa Uno, ngoma mbaya kuliko zote alizowahi kutoa, halafu imekuwa na majanga. Ikanyofolewa YouTube.

DK LEVY: Umetaja wabomoa muziki wote hao. Katika hao waliowasimamia miaka hiyo niambie anayemkaribia hata kwa mbali Konde Boy. Maana unataja watu wote ambao hivi sasa huenda wanauza vitunguu huko Ruaha Mbuyuni.

Fella na Tale wamemkuta Mondi yuko mbali sana. Nakuambia tu kwa faida yako Mondi anawaongoza wanaotakiwa kumuongoza. Nature alifika wapi akiwa na Fella? Madee alifika wapi akiwa na Babu Tale? Tip Top Connection na TMK Wanaume walifika wapi wakiwa na hao jamaa zako?

Wakati mwingine mnawapa sifa wasizostahili. Wale wapo pale kwa ajili ya fitna na imani za Mswahili na Uswahili wake. Muziki ni biashara inayohitaji hesabu za kisayansi.

Lakini kwa kuwa mmezoea biashara zile za enzi za kina Mbaraka Mwishehe ndo maana mnaona hao ni watu wa maana. Fela na Tale wanafanya mipango ya Simba na Yanga wakati muziki unahitaji mipango ya ‘Kibaselona’.

Mnawapa vichwa bure kabisa hao Waswahili. Wana maeneo yao wanayofanya kweli kama kuzuia mvua siku ya shoo na vitu kama hivyo ila siyo mengine haya yanayohitaji elimu ya darasani na fursa.

LUQMAN: Tatizo lako la miaka yote kila ukiambiwa kitu unabisha. Haya jibu na hili, Mbwana Samatta huwa anakosa magoli au anajikosesha? Zingatia ni wapi kaitoa Taifa Stars. Usisahau kuoanisha wachezaji wa Genk na Stars. Hakikisha unawekamo tashwishwi na tashtiti

DK LEVY: Tuna tatizo kubwa kuliko watu wanavyofikiria. Samatta anawaza kusajiliwa zaidi Januari na timu za Uingereza kuliko kushiriki AFCON. Akiumia leo atasajiliwa NIDA au BASATA labda. Hatua tuliofikia ya usugu wa tatizo ni vigumu kupata tiba. Maana hatujui tunataka nini ndo maana hatuelewi Samatta anachofanya. Tungekuwa tunajua tuachotaka pia tungejua Samatta anachofanya ni kwa sababu ya anachotaka.

Yaani Tanzania inahitaji kubatizwa na kuzaliwa upya, tena ule ubatizo wa Kisabato wa kuzamishwa kwenye maji mengi, ndipo tutaweza kuamka kutoka kwenye usingizi wa pono.

Nafuu pekee tuliyonayo ni kuwekeza katika kizazi kijacho, watoto wetu! Wafundishwe tulipotoka! Wafundishwe tulipokosea! Ndo maana hatumuelewi Samatta. Sasa unataka Samatta ajitutumue kama kifutu huku akiwa amezungukwa na wachezaji wanaowaza kuchezea Yanga au Simba kisha wastaafu.

TFF wataweza kumtibia kweli huku wakiwa wameshindwa kumjumuisha Shomari Kapombe ili apate haki yake ya milioni 10 na kiwanja Dodoma?

Watoto wetu wafundishwe wajue kwanini sisi hatuwezi kuchukua hatua kuifanya Tanzania iwe nchi ya Neema!

Wafanye mapinduzi ya fikra na maamuzi. Sisi tumeshindwa. Hatuwezi kuubadili mfumo unaotuongezea umasikini kila siku. Tumeshindwa! Ndo maana tunamshangaa Samtta anayejituma kwenye timu itakayompa mafanikio zaidi kwenye umri wake ule aliofikia.

Samatta hawazi kucheza Afcon kama ambavyo hakuwahi kuwaza kuchezea Simba na Yanga. Samatta alizaliwa acheze kwa wenye akili sema Mzee Samatta alimzalia hapa kwetu.

LUQMAN: Maelezo meeengi, mareeefu, halafu hata swali hujajibu. Labda nikuulize swali; Shilole ni mama lishe, muigizaji au mwanamuziki?

DK LEVY: Mlezi wa wana. Yaani kama katapila au greda vile. Linachonga barabara ili vijana yaani vigari vidogo vipite. Kwa hiyo ni mjasiriamali mwenye kelele na muunganiko wa maigizo. Ujue kuna kuigiza na maigizo. Maigizo ni kama Steve Nyerere kujifanya Nyerere. Yale ndo maigizo.

LUQMAN: Harmonize kujifanya Diamond sio maigizo? Pole sana, nasikia kaka yako kipenzi Patrick Aussems amesimamishwa kazi. Kama familia mmejadili vipi?

DK LEVY: Mondi naye kujifanya Dangote si maigizo? Na kujifanya Mondi Bin Laden je? Siyo maigizo? Asante kwa kunikumbusha kuhusu Uchebe. Huoni kama Simba kumfukuza Uchebe wamewaiga Yanga waliomfukuza Papaa Zahera? Konde Boy anaiga lakini anaweza zaidi mpaka sasa Mondi ndo anaonekana anaiga kwa Konde Boy...

Mafanikio ya Simba na Yanga ni idadi ya makocha wengi waliopita kwenye klabu hizi. Simba pekee imefundishwa na makocha wengi kuliko idadi ya makombe iliyoshinda toka 2010 mpaka sasa. Simba na Yanga ni kama... . Anaendelea tu, lakini mvuto hakuna.