Safari ya mwisho ya Godzilla ilivyojaa mateso

Muktasari:

  • HICHO ni kipande katika wimbo mpya wa Godzilla ambao unabamba kinoma na kifo chake ni kama kimechochea ngoma hiyo kuendelea kukata anga.

Chezesha local MC kama vile controler,

Na deal na kila level mpaka wale bad

Uki-bling wing I need my dollar,

Huwezi goes in the building homy say halla,

Meli iko salama iko bahari I say,

Ili shughuli ziende so inabidi itembee,

Usiamini hao rafiki they rever been true,

If they change on me, they can change on you,

Be humble my G, check your move I swear,

Usilete mbwembwe mwisho ukaishia kwenye wheelchair,

Unaomba msamaha, don’t look like I care,

Umeharibu michongo yangu, why should I care,

Hata ukisema nini you know I don’t mind,

My crew on the spot let me blow your mind,

Hata ukisema nini, I don’t mind,

My crew on the spot let me blow your mind,

AAAH!

chorus

Naweka X kama unauza siri zangu,

Naweka X jua wewe sio mchizi wangu,

Naweka X kama unauza siri zangu,

Naweka X (ye,ye,ye,ye,ye)

HICHO ni kipande katika wimbo mpya wa Godzilla ambao unabamba kinoma na kifo chake ni kama kimechochea ngoma hiyo kuendelea kukata anga.

Wapo wanaoamini ni kama aliyekuwa staa wa Bongo Flava anayesifika kwa kupiga free style matata, Golden Jacob ‘King Zilla’, ambaye jana Jumatano asubuhi taarifa za kifo chake zilionekana kuwatia huzuni wasanii na mashabiki wa muziki.

Hakuwa mtu wa skendo na mwenye majivuno kama wengine na alianza kujenga jina kwenye Bongo Flava wakati aliposhiriki kwenye shindano la Free Style, ambapo walitokea wasanii Nikki Mbishi, Mkristo, Pop Md na wengineo.

Zilla anaongeza idadi ya wasanii waliobamba kinoma kwenye Free Style ambao, wametangulia mbele ya haki baada ya Mangwair na Langa.

Simanzi kubwa imetanda maeneo ya Salasala na studio za MJ Records ambako ilikuwa ni kama nyumbani kwake kutokana na kushinda na kurekodi ngoma kadhaa akiwa na Mtayarishaji Marco Chali.

Mwanaspoti ambalo liliweka kambi maeneo ya nyumbani kwao Salasala na kukutana na kuzungumza na ndugu, jamaa na marafiki wa Zilla akiwemo dada yake, Joyce ambaye alielezea tukio zima hadi kupatwa kwa umauti kwa mdogo wake huyo.

CHANZO CHA KIFO

Joyce alilieza Mwanaspoti Zilla aliugua ghafla na kukimbizwa kwenye kituo cha afya cha karibu na nyumbani kwao, ambako aligundulika kuwa na malaria pamoja na shinikizo la damu.

“Tulimpeleka Mico Dispensary ambacho kipo huku Salasala, alifanyiwa vipimo na kubainika kuwa na malaria na presha ilipanda, wakamuwekea dripu kwani haikuwa rahisi kutibu vyote kwa pamoja,” alisema Joyce na kuongeza:

“Pia alikutwa na kitu tumboni ambacho akitaka kutapika kama kinataka kutoka, lakini hakitoki na hapo tukarudi nyumbani akiwa amepigwa sindano ya kuzuia kutapika.

AMFATA DADA CHUMBANI GHAFLA

Baada ya kutoka hospitalini na kupatiwa matibabu, Joyce alieleza ilikuwa tayari ni usiku na walikuwa wakijiandaa kulala, lakini ghafla Zilla alishindwa kulala chumbani kwake na kumuomba dada yake walale pamoja.

“Sikuwa nimelala kwa siku tatu hivi hivyo, nilimuomba Mama nilale na kama likitokea lolote basi niamshwe, nikiwa chumbani kwangu mama alinifata na kuniambia naitwa, lakini mara nikamuona Jacob na yeye amekuja.

Aliniambia kuwa anaona watu wengi wakiizunguka nyumba na kumtaka waondoke wote hali ambayo ilimshtua zaidi.

“Alitaka kulala na mimi baada ya kushindwa kulala peke yake, nikabidi nimwambie alale halafu mimi nikae hivyo hawezi kuchukuliwa, lakini bado alishindwa na kuomba kunyanyuka na kutoka nje,”.

AFIA NYUMBANI

Baada ya kushindwa kulala peke yake na katika kitanda cha dada yake, alinyanyuka ghafla na kuomba kutoka nje na alipoulizwa aliomba atolewe nje.

“Ilikuwa kama saa nane za usiku na alikuwa anahangaika sana, tulimshika na kumweka chini, lakini alionyesha kabisa kutokuwa nasi hivyo, ikabidi tumpeleke hospitali,” anaongeza Joyce.

Safari ya kumpeleka hospitali ilishia Hospital ya Lugalo na moja kwa moja akapelekwa wodi ya wagonjwa mahututi (ICU), ambako madaktari baadaye waliwaeleza wanaweza kwenda kumuona lakini, lazima wawe wajasiri.

Hata hivyo, hawakuielewa kwa haraka kauli hiyo ya madaktari, ndio ulikuwa mwisho wa Zilla hapa duniani.

MWASITI NA SHILOLE MAPEMA TU

Mwasiti Almas na Shilole walikuwa walikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio baada ya kupokea taarifa za msiba huo.

Wasanii hawa walifikia moja kwa moja na kwenda jikoni kufanya shughuli za kuweka mambo sawa kabla ya wageni kuanza kufika. Ikumbukwe Godzilla kipindi cha uhai wake, alifanya ngoma ya ‘First Class’ na Mwasiti na ilibamba kinoma. Miongoni mwa nyimbo za King Zilla ni Salasala, Thanks God, X, Get Off my way, pia alikuwa katika hatua za mwisho kuachia ngoma nyingineakiwa na Nikki Mbish na Lady Jaydee.

Zilla, amezaliwa Januari 5, 1998 akiwa ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya mzee Jacob. Zilla ameacha mtoto mmoja nayeitwa Shawn (4).