SALLAM SK ALIVYOZINGUA KUMUIGA MAALIM SEIF

Muktasari:

Sallam SK aligoma kupokea mkono wa salamu kutoka kwa Harmonize katika msiba wa mke wa Babu Tale huko Morogoro.

MENEJA wa WCB, Sallam SK, aliamua kufanya kile ambacho Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, alikifanya mwaka 2016. Wakati wa mazishi ya Rais wa Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, Rais wa Sita wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, alimsogelea Maalim Seif na kumpa mkono, lakini alikataa.

Seif alikuwa akilalamikia kudhulumia ushindi wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu 2015, ambao ulioteshwa mbaya na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, ZEC, Jecha Salim Jecha. Seif akaona Shein ndiye anashikilia urais wake. Kwa hasira akamnyima mkono. Sallam naye ameona sijui Harmonize anashikilia kipi? Naye kamnyima mkono. Luqman Maloto na Dk Levy wapo nawe Kijiweni hapa.

LUQMAN: Yule Harmonize kumbe ni mwiba unaochoma sana pale WCB. Yaani Sallam ameona asijifiche, amnyime mkono. Itakuwa Harmonize kaacha pengo kubwa sana pale WCB, mpaka jamaa wanashindwa kujificha wanaamua kuweka wazi hisia zao.

DK LEVY: Sallam ndio nani?

LUQMAN: Meneja wa WCB.

DK LEVY: Nilishakwambia usiwe unaniletea stori za hao ‘mabichi boy’ wao. Meneja watakuwa wale wakati hawajui chochote. Wale jamaa walihisi Konde Boy anatest mambo, wakati aliamua kweli kulipeleka duniani chama kubwa la Konde Gang. Na hapo ni mwanzo tu. Nini kumnyima mkono, akitaka hata aukate kabisa, sanasana anajichoresha tu. Kunyimana mikono ni mambo ya kishamba. Hata Maalim Seif mwenyewe alishasema hawezi kurudia tena ule ushamba wa kumnyima mkono Dk Shein. Halafu anarudia tena ushamba uleule.

LUQMAN: Unajua nini, matukio yote mawili ya kunyima mikono yametokea misibani. Maalim Seif alimnyima mkono Shein wakati wa msiba wa marehemu Aboud Jumbe. Na Sallam amemnyima mkono Harmonize kwenye msiba wa mke wa meneja mwingine wa WCB, Babu Tale. Kumbe misibani ndio kuna sinema za kubaniana mikono, au sio?

DK LEVY: Unajifanya unajisahaulisha tukio la mfalme uchwara wenu wa Kariakoo. Unasahau Alikiba alimnyima mkono Diamond kwenye msiba wa Agnes Masogange? Kwa kifupi kwenye misiba ndio maeneo mtambuka ya watu kuonesha vinyongo vyao kwa wenzao. Ukimuona Sallam mwambie nimepokea kinyongo chake kwa Harmonize, lakini hakimsaidii kitu. Harmonize atazidi kupanda tu.

LUQMAN: Nikikwambia watu kama Sallam ndio huwa wanakwenda peponi utaamini? Sallam hajataka unafiki, ameona yeye hampendi Harmonize, kwa hiyo hakuwa na sababu yoyote ya kujificha. Aliamua kuweka wazi hisia zake ili nchini na dunia nzima ijue kuwa yeye hampendi Harmonize. Na watu kama Harmonize hawafai, maana chinichini ana kinyongo halafu machoni anataka kujionesha kila kitu kipo sawa. Hayo mambo hayafai mkurungwa. Na suala la Alikiba lielewe vizuri, Ali hakumnyima mkono Diamond. Alimpa mkono akiwa ameugeuza, halafu akaongeza na wa pili, kuonesha unyenyekevu. Ali sio mtu vinyongo na visasi kama ninyi Konde Gang na WCB.

DK LEVY: Kugeuza mkono ndio nini sasa? Yule mfalme uchawara ni miyeyusho tu, hana lolote. Tuongee mambo mengine yenye kuweza kuijaza dunia. Unajua Harmonize mpaka sasa ndiye staa anayeinyima usingizi WCB? Si unaona Rich Mavoko hazungumziwi? Ni kwa sababu hana kitu cha kuitikisa WCB.

LUQMAN: Hiyo tabia ya Sallam kumnyima mkono Harmonize wala haiwakilishi msimamo wa WCB. Mbona Harmonize alipotoa albamu yake, Diamond alikuwa wa kwanza kuipost na kutaka watu waende wakaidownload? Diamond haoni kama Harmonize ni kikwazo kwake. Anampa sapoti yote. Kama Diamond angekuwa ananyimwa usingizi na Harmonize asingempost na kumuombea mashabiki wakaidownload albamu yake.

DK LEVY: Hujawahi kuishi kwenye mtaa wa wenye roho mbaya na wanafiki. Siku zote mnafiki ndio huwa wa kwanza kujionesha hana kinyongo na mwenzake. Anaweza kujitoa kwa kila hali kuonesha watu kwamba yeye ni mtu poa, kumbe ndiye anayepiga misumari ya chinichini. Yule Diamond anampiga sana misumari Harmonize, ndio maana alimdai Sh500 milioni.

LUQMAN: Ulitaka aondoke WCB bure? Acha zako bana. Ukiwa unampenda Harmonize, mshauri aache unafiki wa chinichini, awe anakuwa wazi kama Sallam. Diamond alimpigia debe mitandaoni, lakini hata kusema asante alishindwa. Kuna unafiki mkubwa kuliko huo. Tena ukimuona umwambie kuwa yeye bado sana mbele ya Diamond Platnumz, Chibu Dangote, Simba.

DK LEVY: Na wewe ukimuona Sallam, umwambie aache hizo alizoleta za kizamani ambazo hata Maalim Seif alisema ni ‘ushamba, ambao hataurudia tena.