Queen Suzy karudi kivingine mzigoni

Muktasari:

  • Aidha Suzy alipangua tuhuma zinazosambazwa na baadhi ya watu kuwa Nyoshi anampendelea.

MNENGUAJI tishio wa Bendi ya Bogoss Musica, Suzan Chubwa ‘Queen Suzy’,ambaye aliwahi kuzitumikia Bendi za FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ na African Stars ‘Twanga Pepeta na TOT Plus, amesema alishastaafu kama miaka mitatu iliyopita, ila mashabiki na mkurugenzi wake, Nyoshi Elsaadat walimuomba arudi katika ‘game’.

Suzy ameliambia Mwanaspoti kutokana na maombi hayo hakuwa na ubishi kwani ameona bora awape radha mashabiki wake kwa moyo walioonyesha kuwa bado wanamuhitaji.

“Yaani huwezi kuamini, nilistaafu nikiwa na FM Academia, lakini nikiwa nyumbani mashabiki zangu wakwa wanapiga simu kuniomba nirudi na hata Rais wangu wa Milele, Nyoshi El Saadat alikuja kuniomba.

“Sikutaka kuwatia simanzi mashabiki wangu, kutokana na heshima kubwa waliyonipa kwa kujali kazi yangu, hivyo ndio nikaamua kurudi katika bendi ya baba yangu (Nyoshi), nawapa mashabiki zangu radha nzuri kama kawaida tena nimeongezeka ujuzi,” alisema Queen Suzy.

Aidha Suzy alipangua tuhuma zinazosambazwa na baadhi ya watu kuwa Nyoshi anampendelea.

“Wameshasema sana, lakini ukweli ni kwamba mfanyakazi akiwa vizuri lazima bosi akukubali, hivyo Nyoshi anajua uwezo wangu nikiwa kazini sina utani nathamini kazi yangu,” alisema Suzy.

Suzy alisema kuna tofauti kubwa ya utendaji kazi kati ya Bogos Musica na bendi alizowahi kupitia na anaamini bendi hiyo inaweza kurudisha heshima ya muziki wa dansi na kuwa kama zamani.