Ommy Dimpoz : Afichua alivyopambana kuokoa maisha yake

Muktasari:

  • Ommy anaongea vizuri sasa. Anaimba. Ametoa wimbo mpya ‘Ni Wewe’, ngoma tamu yenye kutoa ushuhuda wa ukuu wa Mungu. Ngoma ya kumpa shukurani Muumba mwenye kusimamia uponyaji.

ALIPOTOKA Afrika Kusini alikofanyiwa oparesheni ya mara ya pili, sauti ikawa haitoki vizuri. Ommy Dimpoz anasema, hata alipokuwa chumbani, alipomwita msaidizi wake aliyekuwepo sebuleni ili ampe msaada, sauti haikufika.

Hofu ikawa je, ataimba tena? Madaktari walimwambia ataimba, maana alifanyiwa upasuaji kwenye njia ya chakula. Mfumo wa sauti haukuguswa. Hata hivyo, ongea yake ikawa inawapa wengi wasiwasi.

Huo wasiwasi wengi waliuficha kwenye nyoyo zao, hawakutaka kuushirikisha umma. Kosa la Steve Nyerere ni kuthubutu kuzungumza katika wakati ambao haukuwa sahihi. Akasema; “Yeye anajua” asingeimba tena. Steve anaonekana ‘mchawi’ leo kwa sababu ya hiyo kauli yake. Ukimsikiliza vizuri Steve si kwamba alikuwa akifurahia Ommy kupoteza sauti, ila alimsikitikia, ndiyo maana alitaka watu wajitoe kumsaidia. Hata hivyo, simtetei sana, maana angeweza kuchagua maneno tofauti ya kufikisha alichokikusudia.

Ommy anaongea vizuri sasa. Anaimba. Ametoa wimbo mpya ‘Ni Wewe’, ngoma tamu yenye kutoa ushuhuda wa ukuu wa Mungu. Ngoma ya kumpa shukurani Muumba mwenye kusimamia uponyaji.

Nimeona interview yake na mtangazaji Milliard Ayo, iliyofanyika kwenye YouTube channel ya OmmyDimpoz. Anasimulia sauti ilivyorudi kuwa ni kabla hajapelekwa Ujerumani alikofanyiwa oparesheni ya tatu.

Anasema, alipigiwa simu na bibi yake, akamwambia ameshahangaika hospitali, kwa hiyo anachotakiwa kufanya ni kumkabidhi Mungu na angemponya. Bibi akampa maelekezo ya kusoma dua na kuchukua maji kisha kuyaombea na kuyanywa. Bibi alimwelekeza Ommy mpaka muda wa kusoma hiyo dua yenyewe.

Ommy alifanya kama alivyoagizwa na bibi yake. Baada ya dua alilala, asubuhi alipoamka, simu ya kwanza kuipokea ilikuwa ya bibi. Ooh, bibi alipomaliza kusali sala ya asubuhi, akampigia simu mjukuu wake kumjulia hali. Ommy akapokea simu. Sauti ikatoka. Bibi akashtuka, akajua kapokea mtu mwingine.

Bibi akasema: “Mpe mwenye simu niongee naye.” Ommy akajibu: “Ni mimi mwenyewe bibi.”

Sauti ya Ommy ikawa imerudi. Na hayo ndiyo mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W) kwa umma wake wa Kiislam kuwa matibabu ya hospitali na dawa zake ni sababu ya kupona ila mponyaji ni Mungu.

MWANAJESHI KASHINDA

Mwaka 2004, waandishi George Stalk na Rob Lachenauer waliandika kitabu “Hardball; Are you playing to play or playing to win?” Yaani Mpira Mgumu; Unacheza kucheza au unacheza kushinda? Kitabu hicho kilikuwemo kwenye machapisho ya Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani mwaka 2004.

Sura ya kwanza ya kitabu hicho, Stalk na Lachenauer wameiita “The Hardball Manifesto.” Yaani Ilani ya Mpira Mgumu. Wanasema kuwa washindi hucheza mpira mgumu siku zote. Wanaeleza kwamba kutafuta ushindi lazima kutumia kila silaha ili kuchukua pointi muhimu.

Ommy amecheza mpira mgumu ili kuyashinda maradhi ambayo yamemtesa kwa muda mrefu na kumwekea kiwingu katika mitikasi yake ya kusaka tonge. Alitafuta tiba Dar es Salaam, akaambiwa ana kansa, akaenda Kenya ambako stori kuwa ama alikula au alikunywa sumu ilianza. Sumu tena! Nani huyo katili aliyempa? Tuyaache kwanza hayo!

Kenya alifanyiwa upasuaji wa kwanza hali bado ikawa si hali. Akaenda Afrika Kusini, akafanyiwa oparesheni ya pili. Ommy akawa mgonjwa hasa. Taratibu akaanza kurejea mtandaoni japo alizungumza kwa sauti bandia. Taarifa mpya zikawa Ommy amezidiwa upya na kupelekwa Ujerumani.

Anasema alipokwenda Ujerumani sauti ilikuwa imeshakaa sawa. Desemba yote akaimaliza kitandani Ujerumani, lakini sasa yupo fiti kimtindo. Ametuma salamu za kurejea kwake kupitia ngoma yake mpya, ‘Ni Wewe’. Hii inafundisha pia kwamba ukiyavuka majaribu, toa shukurani kwa aliyekuvusha; Mungu Mfalme.

Hata Papii Kocha na mzee wake, Nguza Viking ‘Babu Seya’, walipotoka jela kwa msamaha wa Rais, wimbo wa kwanza aliotoa ulikuwa ni; ‘Waambie’, kwamba Mungu awaambie kuwa hata walipokuwa nyuma ya nondo alikuwa akisikiliza maombi yao na wakati ulipofika wakaachiwa huru. Ujumbe ni kutokata tamaa.

Amefanya kile ambacho washindi hufanya. Kutumia kila silaha kuusaka ushindi. Hospitali Afrika na Ulaya pamoja na Mungu. Unaona kabisa alistahili kupona. Amecheza mpira mgumu. Ameyachezea rafu nyingi maradhi yaliyokuwa yakimsumbua. Ameshinda sana.

Kama Abraham Lincoln alivyolala kitandani miezi nane kwa sababu ya maradhi ya mfumo wa neva, lakini alipopona alikwenda kuwa Rais wa 16 wa Marekani, bila shaka Ommy bado analo jukumu la kufanya. Anapo mahali anatakiwa kufika. Mungu amempa nafasi nyingine ili afike. Ameridhika Ommy ni mpambanaji hasa na anaweza zaidi.

KUNA ANAYETESEKA?

Karibu tena kibarazani Ommy. Watanzania wanakupenda na walikuombea sana. Mungu ni sababu ya kila kitu. Hongera kwa ushindi mkubwa ulioupata katika mapambano kati ya afya na maradhi. Hakika, Ommy hajacheza na maradhi ili acheze nayo, ameyachezea mpira mgumu ili kuyashinda. Ameyapiga sana rafu mpaka za mguu shingoni.

Hapa ni kuyapa pole maradhi yaliyomsumbua muda mrefu. Tangu Mei mwaka jana aligeuka mwenyeji wa hospitali. Bila shaka yamepata yalichostahili. Mmh! Pole yake au yao, aliyempa au waliompa sumu. Ni kweli wamemtesa sana, lakini mwisho Ommy ni mshindi.

Kama kweli walimtendea hivyo makusudi, je, lengo lao walitaka afe? Ommy hajafa. Walitamani asiimbe tena? Anaimba sasa. Pengine ndiyo kundi la watu walio kwenye mateso makubwa mno hivi sasa. Wimbo wa Ommy ukipigwa wanateseka, wanatamani kufunga muziki. Wakisikia anahojiwa redioni wanatamani kufunga redio, lakini inabidi wasikilize mpaka mwisho, kwa kuhofia kwamba pengine wameshajulikana, kwa hiyo inawezekana akawataja. Basi wanatega masikio pina kusikiliza mahojiano mwanzo mpaka mwisho, lakini hawataji. Wanapumua kwa shida japo hawana matatizo kiafya.

Wakiingia mitandaoni Ommy anafunika kwa watu kumzungumzia chanya, kuusifu wimbo wake, kumwombea na kumpongeza kwa kuyashinda maradhi. Wanaumia na kutamani wasiingie kabisa mitandaoni.