Nedy ajivunia ubunifu wake

MSANII wa bongo fleva, Nedy Music amesema  hakuna kitu cha kumpa presha  kwenye ushindani wa muziki sokoni, kwasababu anaamini aina  ya uimbaji na vionjo alivyonavyo ndivyo vinavyowavuta mashabiki wake.

Msanii huyo amesema kufahamika kwake, kumetokana na bidii na kuwa mbunifu wa mashairi yake, jambo linalompa ujasiri wakuamini kwamba licha ya uwepo wa wasanii wengi, yeye ana nafasi yake.

"Ukikuta msanii anafanya kazi kwa presha, basi hafanyi mashairi yake kwa ubunifu, ukiwa na kitu chako ukiimba tu watu wanatambua kwamba huyu ni Nedy, lakini ukiwa sio mbunifu ni ngumu kuwa na kitu chakukutambulisha," amesema Nedy.

Ameongeza kuwa "Najua nina mashabiki wangu ambao wanapenda aina ya uimbaji wa mashairi yangu, video zangu ndio maana nafanya kazi kwa kujiamini na utulivu,"amesema.

Amemtolea mfano Mr Blue kwamba alikuwa anampenda wakati yeye akiwa mdogo na kwamba zilikuwa zikipigwa nyimbo zake zilikuwa zikimtambulisha kwamba yeye ni nani.

"Kati ya wasanii ambao nilikuwa nawakubali kuanzia kuimba mpaka uvaaji wake ni Mr Blue, mpaka nilipambana kufanya nyimbo naye, mtu kama huyo huwezi kusema ana presha sokoni kwani ana aina yake ya uimbaji inayokubalika na mashabiki wake,"amesema.

Nedy ameliambia Mwanaspoti Online, Leo Jumatatu ya Oktoba 19, mwaka 2020 kwamba kuna kazi anazifanya anazoamini zitakuja kwa kishinda na mashabiki wake watafurahia kuziona na kuzisikia.

"Naandaa kazi, mashabiki wangu watazifurahia kwasababu sijawahi kuwaangusha, wakae mkao wakula kwani sio muda mrefu nitafanya mambo,"amesema.