Breaking News
 

Nandy Utampenda kiulaini tu

Friday January 12 2018

 

By NASRA ABDALLAH

ALIANZA kama utani, lakini sasa amekuwa mtamu kuliko hata mcharo. Ni mwanadada, Nandy, ambaye sasa anatamba kwenye Bongo Fleva.

Kwanza anapaishwa na sauti yake nyembamba inayopenya kama sindano na yenye uwezo wa kumtoa nyoka pangoni.

Nandy hakuwa anafahamika sana, lakini aliporejea kutoka kwenye mashindano ya kusaka vipaji kule Nigeria miaka miwili iliyopita, alianza kwa kibao ‘Nagusagusa’ kilichotamba kiduchu, lakini sasa mambo yameanza kumnyookea kwenye mstari.

Sauti yake ya dhahabu katika wimbo ‘One Day’ uliompa tuzo ya Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki katika tuzo za Afrimma na kile kibao cha ‘Wasikudanganye’,  imetikisa kinoma.

Mambo ya Nandy yamezidi kuwa mazuri kwani, video yake ya Kivuruge nayo pia  imeendelea kufanya vizuri baada ya kutazamwa na watu zaidi ya milioni 1.2 kwenye Youtube ikiwa ni siku 22 tu tangu ilipotoka.

Video hiyo iliachiwa rasmi Desemba 19, mwaka jana lakini mpaka kufika jana Alhamisi ilikuwa imeshatazamwa na watu 1,227,751 na imeweza pia kushika chati za juu katika vituo mbalimbali vya Redio na Televisheni.

Habari njema zaidi kwa Nandy ni kwamba, baadhi ya wadau wa muziki waliotoa maoni yao kuhusu ubora wa video hiyo wamempongeza kwani ina uhalisia wa maisha ya mwanamke wa Kitanzania.

Video hiyo inamuonesha Nandy akiwa ndani ya dela na kitambaa kichwani, akiishi maisha ya uswahilini ambako pia alikuwa akiuza mboga.

Mdau wa muziki nchini, Francis Daudi, alisema mwanamuziki huyo ametendea haki mavazi yake kwenye video hiyo kwani, inatazamika na watu wa rika zote.

Naye Shakira Purity alisema kilichofanywa na Nandy kimewadhihirishia wasanii wengine hususani wanaopenda kwenda kufanya kazi kwenye nchi za watu kwamba, hata nyumba za uswahilini zinaweza kutoa video bomba na pia kusaidia kuitangaza Tanzania.

“Nimeitazama video hii mara 10, kisha nimemuonesha rafiki yangu mmoja ambaye si Mtanzania akaniambia ni bora na kukiri kwamba, Nandy ana kipaji cha hali ya juu na kuwa kila anapoiangalia anatamani kuendelea kuona mazingira hayo,” alisema Shakira ambaye hakusita kumpa Nandy tano.