NICO MILIMO : Mtoto wa mchungaji anayetesa Sky Melodies

Thursday May 16 2019

 

By Rhobi Chacha

KWA wakazi wa Dodoma na mikoa jirani, Bendi ya Sky Melodies sio ngeni masikioni mwao.

Sky Melodies ni bendi inayoweza kukupa burudani kutokana na wanamuziki wake kuimba nyimbo yoyote unayoitaka. Ni mabingwa wa kupiga ‘kopi’ Dodoma nzima hakuna. Bendi hii inaongozwa na Mwanamuziki Nico Millimo ambaye alianza shughuli za muziki akiwa darasa la tatu akianzia kwenye kwaya za shuleni na kanisani.

Millimo alianza kujihusisha na muziki wa bendi mwaka 2001 akiwa na Bendi ya Saki Stars ya jijini Dodoma, mwaka 2012 alitoka na kuanzisha Bendi ya TCN na mwaka 2015 akaachana nayo na kuanzisha bendi yake ya Sky Melodies.

Mwanaspoti limefanya mahojiano Millimo ambaye historia yake inaonyesha ametoka familia ya uchungaji.

Millimo amefunguka mengi kuhusu bendi yake hiyo ambayo mbali na kupiga kopi pia ina nyimbo zake za Dorice, Faraja, Hapa Kazi Tu, Ahsante, Kwangua Vocha, Shukrani ya Wazazi na Nishike Mkono.

Mwanaspoti: Imewezaje kuchana na Injili hadi muziki wa dansi?

Millimo: Naimba muziki wa dansi kwa saba¬¬bu naupenda. Hata wazazi wangu walikubali kwa sababu walijua ni kitu nilichokipenda na waliamini kwenye ndoto zangu tangu utotoni, kwani nilianza kuonyesha kipaji cha kuimba tangu kanisani.

Mwanaspoti: Changamoto unazozipata katika muziki?

Millimo: Ni ugumu wa kuendesha bendi nikiwa mwanamuziki ambaye nategemea kwa kiasi kikubwa kipato kinachotokana na mapato ya bendi. Nyingine ni tabu ya wanamuziki kutotulia sehemu moja unaweza kumtegemea mkashirikikana vizuri siku chache akaondoka, kwa hiyo inarudisha nyuma kiwango cha bendi. Pia, media kutupa kipaumbele muziki wa dansi lakini hata wanaotupa sapoti wanakosa waendeshaji (watangazaji) wanaoujua muziki huo. Nyimbo nyingi mpya zinatoka lakini watu wanacheza nyimbo za zamani tu.

Mwanaspoti: Kumekuwa na mfumko wa bendi nyingi Dodoma mnakabiliana nalo vipi?

Millimo: Unajua bendi nyingi sio bendi za ukweli. Nyingi ni kama vikundi tu vya kuganga njaa. Kwa sababu aina na uanzishwaji wake ni wa kiwango cha chini kiasi hata wadau hawawezi kuweka akilini kama kuna bendi imeanzishwa

Bendi ni ile iliyoenea sehemu zote muhimu na iliyo na programu yenye kueleweka inayowavutia mashabiki kuifuatilia na kutoa kazi zake. Hizi nyingine zinakuwa hazina utimamu kamili na hata programu hazieleweki.

Mwanaspoti: Kwa nini bendi za mikoani hazifanyi kazi nje ya mikoa yao?

Millimo: Sky Melodies kufanya shoo nje ya Dodoma ni mpaka tutakapojieneza kikamilifu kwenye burudani. Huko mbeleni tutafanya kazi sehemu nyingine. Kwanza tunaisaka fursa ya kupambana kwenye soko. Huwezi kufanya shoo sehemu hujulikani, acha tufanye kazi halafu shoo zitakuja tu.

Mwanaspoti: Mwanamuziki gani unayemkubali hapa Bongo?

Millimo: Namkubali sana Rogert Hegga ‘Katapila’ kwa hapa Bongo. Kwa nje wakati naanza muziki nilikuwa namfuatilia kwa karibu Werrason Ngiama.

Mwanaspoti: Una ushauri nini wanamuziki?

Millimo: Ushauri wangu ni kutulia na kupanga mikakati ya namna ya kupenya kuyatafuta malisho mazuri, sababu karibu bendi zote hazitofautiani kipato na hata uendeshwaji wake. Kwa hiyo ni wakati wa kuchanganya vichwa kwa pamoja na kupambana.

Mwanaspoti: Unautumiaje muda wako wa mapumziko?

Millimo: Kupanga mipango mbalimbali ya bendi na ya kimaisha kwa ujumla, pia kupata mawazo za kutunga nyimbo mpya.

Advertisement