Mwijaku kusomewa maelezo yake Novemba 30

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Novemba 30, 2020 kumsomea hoja za awali (Ph) mtangazaji wa Clouds, Mwemba Burton (35), maarufu kama Mwijaku.

Ni baada ya upelelezi wa kesi ya kusambaza picha za utupu, inayomkabili mshtakiwa huyo, kukamilika.

Mwijaku, ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach, anakabiliwa na shtaka moja la kusambaza picha za utupu kinyume cha sheria.

Wakili wa Serikali, Yusuph Abood ameieleza mahakama hiyo, leo Oktoba 19, 2020 mbele Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

"Kesi hii ilipangwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali, lakini bado hatujamaliza kuchapa taarifa zilizopo katika jalada, hivyo tunaiomba mahakama hii ipange tarehe nyingine," alidai Wakili Abood.

Hakimu Kabate, baada ya kusikikiza maelezo ya upande wa mashtaka, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 30, 2020, ambapo mshtakiwa atasomewa hoja za awali.

Mwijaku yupo nje kwa dhamana, baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.

Katika kesi ya msingi, Mwijaku anakabiliwa na kesi ya jinai namba 110/2020.

Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Septemba 17, 2019 na Oktoba 2019 katika jiji la Dar es Salaam.

Mwijaku anadaiwa kuchapishwa picha za ngono kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp uliounganishwa katika kompyuta.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kusambaza picha hizo, wakati akijua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.