Mwigizaji Tino aja na mbinu mpya kuuza filamu

Muktasari:

 

  • Soko la filamu Tanzania linaonekana kufa kutokana na wadau kudai filamu na wasanii hawana ubora katika kazi zao na ndio maana wanafuatilia filamu za kutoka nje ya Tanzania.

WACHEZA filamu Tanzania, Frank Makundi, maarufu 'Tino'

na mwenzake Grace Mapunda 'Mama Kawele' wamezindua filamu mpya ya Nyavu ambayo itakuwa ikioneshwa kupitia mtandao wa Kwese Inflix kwenye TV 1 na siyo katika CD, kama ilivyozoeleka.

Tino alisema amefurahi kuachia filamu hii mpya ya Nyavu ambayo itakuwa inakwenda kwa mwendelezo ambayo naweza kusema itakuwa imekuja kivingine katika tasnia hii kwani haitaoneshwa kupitia CD, bali itaonekana dunia nzima kwa kupitia mtandao wa Kwese Inflix.

"Kilichotufanya tusiweke katika CD, ni kuogopa kuibiwa kwani tunatuamia pesa nyingi katika kuandaa na mpaka kutengeneza filamu lakini kuna watu wanakuja kunyonya kazi zetu bila ya kutua malipo yoyote na wanakwenda kuuza na kunufaika wao," alisema.

"Dunia imekuwa kubwa nimeona filamu hii ili niweze kupata faida ya pesa na muda uliotumika ni kuiweka mtandaoni lakini kuiona lazima upitie Kwese Inflix ili pesa ambazo watakuwa wanakatwa ambao wanaangalia ndio itakuwa faida kwetu," alisema Tino ambaye aliongezea kuwa yupo katika tasnia ya filamu zaidi ya miaka 20, lakini faida kaanza kupata miaka miwili iliyopita.

Mama Kawele alisema filamu ya Nyavu mbali ya kuja kivingine katika usambazaji wake ambao watapata nafasi ya kuona watajifunza mambo mengi kutokana na ubora uliokuwa ndani yake.

"Kwanza naona filamu inakwenda kupiga hatua kutokana na mfumo huu ambao tumekuja nao wa kuona kupitia Kwese Inflix kwani tutapata kipato stahiki na kuweza kupata maendeleo ya kimaisha tofauti na ilivyokuwa zamani kuona kupitia CD," alisema Mama Kawele.

Nae Meneja Mkuu wa Kwese, Mgope Kiwanga alisema, "Njia ambayo wameitumia wasanii hao kuzindua na jinsi ya kuangalia filamu ya Nyavu itakuwa na faida kwao kwani kila kitu kitakuwa kinaonekana mtandaoni na wao wamekuwa wakionesha filamu kubwa na nyingi katika nchi kubwa."