Mwanamuziki Victoria Kimani atamani kuolewa, akifichua anaogopa mafisi!

Muktasari:

Victoria kasisitiza kuwa kamwe hawezi kutoka na mwanamume asiye na hela lakini hata zaidi asiye na akili za kibiashara

MWANAMUZIKI Victoria Kimani amefichua kuwa anatamani sana kuolewa na kujaliwa watoto ila tatizo ni kuwa wanaume wengi wanaomtokea ni mafisi.

Kichuna huyo  mwenye miaka 34 kwa sasa, kawa singo kwa muda wa miaka miwili sasa toka alipoteana na mpenziwe wa zamani Mnigeria Stanely Obiamulu aishiye Afrika Kusini.

Toka kipindi hicho Kimani kawa singo na ijapo amekiri kutamani kumpata mpenzi, imekuwa shughuli.

“Kuna mwanamume ninayemzimikia kishenzi na ningetamani kutoka na yeye,  ila nafikiri yeye hapendi kuwa na mimi. Maisha yangu ya mahusiano ndio kama hivyo yamekufa zamani,” alitanguliza kusema.

“hata hivyo natamani sana kuwa na familia, nimlee mwanangu katika nyumba iliyo na baba sababu maisha ya kuwa peke yangu siwezi, nitachizi. Ila sasa tatizo ni kwamba sijampata mwanaume kamili, wengi hawa waongo tu. Wanakuwa sio wakeli na maisha yao. Hivyo nipo radhi kusubiri hadi nitakapompata  yule tutakayesitiriana maisha” alisema.

Pamoja na yote, Victoria kasisitiza kuwa kamwe hawezi kutoka na mwanamume asiye na hela lakini hata zaidi asiye na akili za kibiashara.