Mutombo: Changamoto ndio zimenifikisha hapa

Muktasari:

  • Junior Gringo kwa sasa amesharekodi nyimbo kadhaa na kutoa video ya wimbo wake wa Eva, alisema chanzo cha kurekodi nyimbo mfululizo ni kutokana na kumiliki studio yake binafsi na lengo lake kubwa ni kuonyesha uwezo wake kwa mashabiki.

ALIYEKUWA na kiongozi wa Bendi ya Kalunde, Junior Mutombo ‘Junior Gringo’, amesema hakuondoka katika bendi hiyo kwa kupenda pamoja na kudumu kwa takriban miaka minne.

Junior ambaye kwa sasa yuko na bendi yake ya TK Vibration na anatamba na Wimbo wa Eva, alisema kulikuwa na changamoto nyingi za kiuongozi kwenye bendi yake hiyo ya zamani.

“Nashukuru kupokelewa vizuri na mashabiki wangu tangu nimeanza kujitegemea na nilipokuwa Kalunde Band tuliweza kufanya mambo mengi hadi kupata Tuzo za Kili Music Awards mwaka 2010.”

Junior Gringo kwa sasa amesharekodi nyimbo kadhaa na kutoa video ya wimbo wake wa Eva, alisema chanzo cha kurekodi nyimbo mfululizo ni kutokana na kumiliki studio yake binafsi na lengo lake kubwa ni kuonyesha uwezo wake kwa mashabiki.

“Niliachana na kazi za bendi za watu na kuanzisha bendi yangu kwa ajili ya kujiimarisha na sasa naendelea kuzirekebisha nyimbo zangu nilizorekodi siku za nyuma ili nianze kuziachia, ” alisema mwanamuziki huyo.