Mr Blue: Ubunifu unaondoa presha kwenye muziki

Muktasari:

Msanii wa bongo fleva, Mr Blue amesema wasanii kuiga kila kitu kwenye kazi zao ni sababu ya kufanya kazi zao kwa presha.

MSANII wa bongo fleva, Khery Sameer 'Mr Blue' amesema hakuna kitu kinachoweza kumuumiza kichwa kwenye kazi zake kutokana na ubunifu wa muziki anaoufanya.

Mr Blue amesema wakati anaanza kufanya muziki hakutaka kuiga staili ya wanamuziki waliokuwa wanatamba kwa kipindi hicho bali alijitambulisha yeye kama yeye.  

"Asilimia kubwa ya wasanii wengi wanaiga aina ya muziki wa wengine, wakati naanza kufanya muziki nilikuwa mimi, hilo linanisaidia mpaka leo, nikiimba wanajua ni Mr Blue anaimba,"

Ameongeza kuwa "Ubunifu umekuwa adimu kwa wasanii wengi ndio maana kazi zinakuwa hazidumu kwa muda mrefu baada ya muda mfupi zinasahaurika,"

Amesema licha ya uwepo wa chipukizi wanaokuja kwa kasi amekuwa akifanya 'shoo' kama kawaida ndani na nje ya nchi na anaona jinsi ambavyo mashabiki wake wanapenda kazi yake.

"Nikipanda jukwaani mashabiki wangu wanapenda muziki, wanakuwa wananishangilia nakuimba pamoja na mimi ni kiasi gani wanakuwa wanapata muda wa kuzisikiliza nyimbo zangu na kuzikariri,"amesema.