Mpiganaji Ruge kumaliza mwendo wake Bukoba

Muktasari:

  • Hata hivyo baada ya zoezi hilo la kuagwa kuhitimishwa juzi, asubuhi ya jana mwili huo ulisafirishwa kwa Ndege hadi Bukoba ambapo uliwasili saa 4 asubuhi kabla ya kuanza msafara wa kuelekea nyumbani kwa marehemu kijijini kwao.

MWANADAMU huzaliwa mara moja tu, kadhalika hufa pia mara moja kama ambavyo aliyekuwa Meneja wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba aliyezaliwa mwaka 1970 na leo Jumatatu atahitimisha safari yake dunia atakapozikwa kijijini kwao Kiziru, Bukoba Vijijini.

Ruge alikumbwa na mauti Februari 26, akiwa kwenye matibabu nchini Afrika Kusini na mwili wake kurejeshwa nchini Ijumaa iliyopita kabla ya juzi Jumamosi kuagwa kwa heshima kwenye ukumbi wa Karimjee na jana Jumapili ukasafirishwa hadi Kagera na kuagwa tena leo kwenye viwanja vya Gymkhana kabla ya kuzikwa.

Katika hafla ya kuagwa juzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk John Magufuli, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete na mkewe, Mama Salma pamoja na wanasiasa wengine waliwaongoza waombolezaji wengine kumuaga mwili wa Ruge wakiwamo wasanii na wanamichezo mbalimbali maarufu.

Hata hivyo baada ya zoezi hilo la kuagwa kuhitimishwa juzi, asubuhi ya jana mwili huo ulisafirishwa kwa Ndege hadi Bukoba ambapo uliwasili saa 4 asubuhi kabla ya kuanza msafara wa kuelekea nyumbani kwa marehemu kijijini kwao.

Mamia ya wakazi wa Bukoba walijitokeza kwa wingi kuupokea mwili huo na kuusindikiza kwa heshima zote, ambapo ukiondoa gari lililobeba jeneza kuwa na kibao kilichoandikwa R.I.P Ruge, lakini magari yaliyokuwa kwenye msafara yalikuwa na kibao cha Msiba.

Mbali na magari na waenda kwa miguu msafara huo wa mwili wa Ruge ulikuwa na waendesha bodaboda na barabarani waombolezaji wakiwa wamejipanga kwa majonzi.

Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi ya Ruge, leo kuanzia asubuhi mwili huo utaagwa kwenye Viwanja wa Gymkhana kabla ya jioni kuzikwa kijiji cha Kiziru kuhtimisha safari ya mwisho ya Ruge aliyoitumikia kwa zaidi ya miaka 49. Ruge alikumbwa na mauti akiipigania roho yake Afrika Kusini ikielezwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la figo akiwa ameacha watoto watano, akiwamo mkubwa Mwachi ambaye juzi aliwaliza waombelezaji alipomuombea msamaha baba yake kwea wote aliwakosea huku akieleza anawasamehe pia waliomkosea baba yake enzi za uhai wake.

Wadau mbalimbali wa burudani na michezo na hata viongozi na wanasiasa wamekuwa wakimuelezea marehemu Ruge kama mfano wa kuigwa ndani ya jamii kwa namna alivyojitolea kwa hali na mali kuwasaidia wenye vipaji. Enzi za uhai wake licha ya kuchangia kwa sehemu kubwa kukuwa kwa muziki wa kizazi kipya, lakini ni mmoja aliyehusika kulifanya Tamasha la Simba Day lililoasisiwa na uongozi wa Hassan Dalali kuwa lenye mvuto ndani na nje ya Tanzania.