Mike Tyson akaunti zinapumua pesa ,warembo walimtambua

Muktasari:

Pambano la Tyson na Tucker lilikwenda raundi 12 kisha majaji wote watatu walimpa ushindi Tyson kwa unanimous decision. Kwa ushindi huo, Tyson aliweka rekodi ya kuwa bondia wa kwanza wa uzito wa juu duniani, kubeba mikanda yote mikubwa mitatu kwa wakati mmoja, yaani WBC, WBA na IBF.

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya ya maisha ya bingwa wa zamani wa ngumi za uzito wa juu duniani, Mike ‘Iron’ Tyson, tuliangazia alivyoanza hadi kutwaa ubingwa wa dunia akishinda mapambano 28 mfululizo. Twende tena.

Mei 1986, Tyson alifanikiwa kutetea mikanda yake ya WBC na WBA kwa kumtwanga bondia Pinklon Thomas kwa KO raundi ya sita. Miezi mitatu baadaye, yaani Agosti Mosi, Tyson alimkabili aliyekuwa bingwa wa ngumi uzito wa juu duniani, mkanda wa Shirikisho la Kimataifa la Boxing (IBF), Tony Tucker.

Pambano la Tyson na Tucker lilikwenda raundi 12 kisha majaji wote watatu walimpa ushindi Tyson kwa unanimous decision. Kwa ushindi huo, Tyson aliweka rekodi ya kuwa bondia wa kwanza wa uzito wa juu duniani, kubeba mikanda yote mikubwa mitatu kwa wakati mmoja, yaani WBC, WBA na IBF.

Agosti Mosi alimpiga Tucker na kuweka kibindoni mikanda mitatu mikubwa ya Boxing duniani, miezi miwili baadaye, yaani Oktoba, Tyson alijaribiwa na mshindi wa medali ya dhahabu katika Olimpiki ya mwaka 1984, Tyrell Biggs. Ikaaminika lingekuwa pamoja gumu kwa Tyson. Haikuwa hivyo, mnamo raundi ya saba, Biggs alilamba sakafu na kumwacha Tyson akiendelea kutesa kwenye ulimwengu wa ubabe, umashuhuri na utajiri wmkubwa. Alikuwa mwanamichezo aliyekuwa akiingiza fedha kwa haraka zaidi kuliko mwingine yeyote kabla na katika wakati wake.Ni kipindi hicho, Rais wa kampuni ya Kijapan ya michezo ya video (Video Games) ya Nintendo, Minoru Arakawa, alivutiwa na Tyson kwa nguvu zake nyingi na ujuzi wake mkubwa wa kupigana, akaamua kuingia mkataba wa kutengeneza video game ya Tyson iliyoitwa Mike Tysons Punch-Out ambayo ilipata mafanikio makubwa. Nakala zaidi ya moja milioni zilinunuliwa.

Mwaka 1988, Tyson alipigana mapambano matatu. Hata hivyo, kumbukumbu kubwa zaidi ni ushindi wake wa KO raundi ya nne, dhidi ya bingwa wa zamani wa Boxing uzito wa juu, Larry Holmes, Januari 22, 1988. Ni kumbukumbu kubwa kwa sababu kabla ya kupigana na Tyson, mtu mzima Holmes alikuwa hajawahi kupigwa kwa KO katika mapambano yake 75 aliyocheza. Mpaka Holmes alipostaafu masumbwi, pambano pekee alilopoteza kwa KO ni hilo dhidi ya Tyson.

Miezi miwili baada ya kumtwanga Holmes, Tyson alisafiri mpaka Tokyo, Japan na kumkabili bondia Tony Tubbs. Kazi haikuwa ngumu sana, kwani katika raundi ya pili tu, Tubbs alirudisha chenji kwa kukubali kulamba sakafu baada ya kupokea ngumi nzito ya Tyson. Miezi mitatu baadaye, yaani Juni 27, 1988, Tyson alikuwa kazini dhidi ya Michael Spinks. Kipindi hicho Spinks alikuwa moto na hakuwa amewahi kupigwa katika michezo yote aliyopanda ulingoni. Rekodi nyingine ni kuwa Spinks ndiye aliyempokonya mkanda wa uzito wa juu Holmes katika pambano la raundi 15.

Kutokana na sifa nyingi za Spinks, pambano hilo la Tyson na Spinks ndiyo lililoweka rekodi ya thamani kubwa zaidi katika mchezo wa Boxing. Tambo zilikuwa nyingi. Mpaka wakati huo, hakuna bondia ambaye alikuwa ameshapigwa kwa wote wawili.

Spinks alikuwa akitamba kuwa yeye ndiye bingwa isipokuwa waandaaji wakubwa wa masumbwi walikuwa wakimbania. Sasa kazi ikawa moja kwake kumpiga Tyson na kutangazwa kuwa bingwa wa dunia mbele ya umati na dunia nzima ishuhudie. Matarajio ya pambano hilo yalikuwa makubwa kupita kiasi. Hata hivyo, kila kitu kilikuwa chini ya matarajio, kwani upinzani ambao ulitarajiwa ungeonekana haukuonekana. Tyson alimtwanga Spinks katika raundi ya kwanza sekunde ya 91. Hicho kikawa kichapo cha kwanza kwa Spinks katika historia yake Boxing. Ni wakati huo sasa Tyson akaonekana ni bad-man hasa ulingoni.

Tyson akawa mtu wa kuogopwa lakini ndiye bondia ambaye mapambano yake yalikuwa yanatengeneza fedha nyingi.

Unafahamu kilichotokea hadi akafilisika na maisha yake kwa sasa unayatambua vyema. Jamaa anapiga pesa lakini, kwa familia humwambii kitu. Itaendelea kesho Jumapili.