Mike Tyson : Umaskini kando,sasa ni bata tu!

Muktasari:

Ukiwa kijana unaamini kila mwanamke anaweza kuwa wako. Unaota njozi nyingi na kujiumbia dunia yako. Unaamini hakuna kama wewe na unapita ukitamba. Ukimtaka mwanamke na akikukataa unaweza kumbaka, ukamtukana au hata kumpiga. Ujana ukikutawala unaweza kuvunja sheria za nchi mchana kweupe.

UJANA unapendwa sana lakini unatesa. Ujana haujawahi kutosha. Ukiwa kijana huoni jambo gumu, kila kitu ni chepesi. Unaweza kuwa na mamilioni ya fedha wala usiyapeleke benki. Utayatumia yote kwa kiburi kuwa utapata nyingine. Nguvu ya kutafuta bado ipo.

Ujana ni jua kali. Linavyowaka kwa bidii hadi kuchoma na kuunguza, hutawala anga na nchi, hufukuza mawingu na giza. Likiachwa na utawala wake, huweza kuigeuza nchi yote kuwa ardhi kame.

Kama jua ambavyo hukausha ardhi na kuipa ukame, ndivyo na ujana hukausha mifuko ya kijana mwenye ujana wake. Kijana anaweza kutengeneza mifereji ya fedha, mamilioni yakawa yanatiririsha ngawira kuingia kwenye akaunti zake benki, lakini ujana ukakausha mifereji mpaka fedha benki. Ujana si wa kuuendekeza lakini ni mzuri sana. Ukitembea barabarani ni mwenye afya, unaweza kuutumikisha mwili vyovyote unavyotaka, ukiamua kutokulala kabisa inawezekana na husikii japo maumivu ya kichwa.

Unatembea barabarani wanawake wazuri wanakwita handsome. Unakatiza mitaa vijana wazuri wanakutamka kuwa wewe ni mrembo. Ukijiangalia kwenye kioo huoni mikunjo ya ngozi halafu unajikubali. Ujana ni wakati mzuri zaidi katika maisha ya binadamu.

Kijana anaweza kubadili wanawake atakavyo. Akacheza nao watano na kuendelea kwa siku moja na akawatosheleza bila hata kuongeza nishati kwa dawa za Kichina au Viagra na Super-Shaft. Ujana unapoondoka, ndipo anajikuta aliuchosha mwili na amekuwa dhaifu asiyejiweza.

Ukiwa kijana unaamini kila mwanamke anaweza kuwa wako. Unaota njozi nyingi na kujiumbia dunia yako. Unaamini hakuna kama wewe na unapita ukitamba. Ukimtaka mwanamke na akikukataa unaweza kumbaka, ukamtukana au hata kumpiga. Ujana ukikutawala unaweza kuvunja sheria za nchi mchana kweupe.

Mrembo anapita barabarani kwa kujiamini. Vijana kwa wazee wanageuza shingo kumtazama. Anavutia hasa, akiamua anaweza kuwachezesha wanaume sarakasi anavyotaka. Anaweza kuutumia mwili wake kuishi. Akiwa na uthubutu anaweza kuonja kila mwanaume anayetokea mbele yake. Mwili unampa jeuri.

Jambo moja ambalo lipo dhahiri ni kuwa ujana humaanisha kikomo cha kufikiri. Anaweza kuwa kijana mwenye akili nyingi lakini ujana hufupisha uwezo wa kufikiri, matokeo yake akafanya mambo kwa ujana. Siku umri ukimtupa mkono ndiye anakuwa mshauri bora kwa jamii.

Usiombe kijana apate fedha kisha ziondoke akiwa kijana, anaweza kuwaza kila jambo baya. Si ajabu akajinyonga, akawa mtumia dawa za kulevya au jambazi sugu. Ukiwa kijana hudhani kukosa ni kushindwa na siyo matokeo. Ujana unavimbisha kichwa na kufubaza ubongo.

MABILIONI YA TYSON

Mei 23, 2017, tajiri aliyeukwaa umilionea kupitia mchezo wa ngumi kwa halali kabisa, Mike Tyson, alipokuwa kwenye mahojiano kupitia jukwaa la Salt Conferenze na kuoneshwa na Televisheni ya CNN, alisema: “Sikudhani kama ningeuvuka umri wa miaka 30.”

Tyson mwenye umri wa miaka 52 hivi sasa, alisema kuwa wakati akiwa na umri wa miaka ya 30 alijua angekufa kwa sababu alikata tamaa ya maisha, kila kitu kilegeuka juu chini, akawa mnywaji wa pombe kupita kiasi, mvuta bangi na mnusaji wa dawa za kulevya.

Unadhani kwa nini Tyson alikata tamaa ya maisha? Jawabu ni ujana. Ni kwa nini hivi sasa ametulia na ni mwenye amani mpaka anajishangaa alivyochanganyikiwa alipokuwa na umri wa miaka 30? Jibu lake pia ni ujana. Ni kwamba Tyson kutokana na ujana wake alijiona amefeli maisha baada ya kufilisika.

Je, ni kwa nini Tyson alifilisika? Jawabu ni lilelile; ujana. Tyson akiwa na umri wa miaka 20, tayari ni bingwa wa ngumi katika uzito wa juu duniani. Akiwa na umri wa miaka 15 anachukua medali ya dhahabu katika Mashindano ya Olimpiki Chipukizi (Junior Olympic Games) kisha akatwaa tena nishani ya dhahabu akiwa na umri wa miaka 16 katika michuano hiyo.

Katika Junior Olympic, mpaka leo Tyson ndiye mwenye rekodi ya kushinda pambano mapema zaidi. Alimtwanga bondia, Kelton Brown katika raundi ya kwanza, sekunde ya nane. Katika mapambano yote ya Junior Olympic, Tyson aliwakalisha wapinzani wake wote kwa knockout (KO).

Tyson alikuwa kijana mwenye nguvu na alijielewa, aliutumikisha mwili wake kwa mazoezi na wenyewe ulikubali. Akiwa na umri wa miaka 18, alizipiga teke ngumi za ridhaa na kuanza kucheza ngumi ya kulipwa.

Machi 6, 1985, Tyson alipanda ulingoni kwa mara ya kwanza Albany, New York, Marekani. Bondia wa kwanza kuonja makonde ya Tyson katika ngumi za kulipwa ni Hector Mercedes, aliyelamba sakafu raundi ya kwanza.

Ni baada ya hapo, Tyson alipigana mfululizo katika mwaka wake wa kwanza. Hesabu zinaonesha kuwa mwaka 1985 alipigana mapambano 15. Kwa vile alianza kupigana Machi, hivyo ni kwamba alipigana mapambano 15 ndani ya miezi tisa. Na huo ni wastani wa pambano moja kila baada ya wiki mbili na siku nne.

Kuelekea kuutwaa ubingwa wa ngumi katika uzito wa juu duniani, Tyson alipigana na kushinda mapambano 28, katika hayo, 26 alishinda kwa KO na TKO. Hapohapo ni kuwa mapambano 16 alishinda raundi ya kwanza. Hii ni rekodi ambayo haipo kwa bondia mwingine yeyote kuwahi kutokea duniani.

Unaweza kuachana na habari za Tyson kumvunja pua bondia mkali, Jesse Ferguson katika raundi ya tano Februari 16, 1986 katika Uwanja wa Houston Field Marshal, Troy, New York, na asiwepo mtu wa kukupa lawama, maana vichapo vya Tyson ni vingi mno.

Hata hivyo, kumbukumbu muhimu ni kuwa Novemba 22, 1986, Tyson akiwa na umri wa miaka 20 na miezi minne, alimtwanga Trevor Berbick na kutwaa ubingwa wa dunia, uzito wa juu mkanda wa Baraza la Boxing Duniani (WBC). Tyson alimalizana na Berbick raundi ya pili kwa pambano kumalizwa na refa, yaani TKO.

Akiwa kijana mwenye umri wa miaka 20, miezi minane na siku saba, Tyson mwenye moto wake, alimkabili aliyekuwa bingwa wa dunia mkanda wa Chama cha Boxing Duniani (WBA), James Smith. Pambano hilo lililofanyika Las Vegas, Nevada, Machi 7, 1987, Tyson alishinda kwa pointi kwa uamuzi wa majaji wote, yaani unanimous decision.

Kwa ushindi huo, Tyson akawa amefanikiwa mambo mawili kwa wakati mmoja, kwanza ni kutetea mkanda wake wa WBC, kisha akautwaa kwa mara ya kwanza mkanda wa WBA uliokuwa unashikiliwa na Smith. Hiyo ikawa rekodi ya kijana mdogo zaidi kufikia mafanikio hayo.

Ni wakati huo sasa, mashabiki vindakindaki wa Tyson (Tyson Mania), walipofurika kila kona. Thamani yake ikapanda, hivyo kuanza kusaini mapambano na matangazo kwa fedha nyingi, siyo tu kuliko bondia yeyote katika historia, bali kuliko mwanamichezo yeyote kupata kutokea duniani mpaka kipindi hicho.

Usikose Mwanaspoti kesho uone mambo zaidi ya Tyson.