Mediocre ya Alikiba inazungumzia haya

KWA sasa msanii Alikiba anagonga vichwa vya habari na kuteka mazungumzo mtandaoni mara baada ya kuachia wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la Mediocre. Wimbo huu umegusa hisia za wengi, sio mashabiki wake pekee, hata wasio wake wanatoa hisia zao za ndani zaidi kwa namna walivyoelewa.

Makala haya yanaangazia mambo matano yaliyochomoza mara baada ya kuachiwa wimbo huo.

1. Kubaniwa RockStar Africa?

Wakati Alikiba akiwa chini ya RockStar Africa alikuwa sio msanii wa kutoa nyimbo kila mara, mathalani Agosti 2017, wakati anaachia wimbo wake wa Seduce Me ilikuwa ni baada ya ukimya wa mwaka mmoja.

Tangu ameondoka RockStar Africa yake Seven Mosha na kuanza kufanya muziki chini ya lebo yake ya Kings Music, Alikiba amekuwa msanii wa kutoa nyimbo kila mara.

Kwa mwaka huu tangu uanze ameachia nyimbo tatu ambazo ni Dodo, So Hot na Mediocre. Tangu Alikiba aliporudi kwenye muziki (comeback) Desemba 2014, huu ndio mwaka alioachia ngoma nyingi zaidi.

Ikumbukwe mwaka bado mwaka haujaisha na ana uwezo wa kutoa ngoma nyingine zaidi. Kwa muktadha huo huenda zikaibuka hisia kuwa RockStar Africa ilikuwa kikwazo kwa Alikiba kutoa nyimbo kila wakati.

2. Jibu Mondi

Agosti 21, 2017 Diamond Platnumz alimchana haswa Alikiba kupitia wimbo wa Fid Q uitwao Fresh Remix ambapo alishirikishwa pamoja na Rayvanny. Kiba hakuwahi kujibu michano hiyo kupitia wimbo wowote. Lakini kupitia Mediocre, Kiba amejibu hilo baada ya miaka zaidi ya miwili, kivipi?

Mosi: Kiba amechana (sio kuimba) kwenye verse ya kwanza kama alivyofanya Diamond kwenye Fresh Remix. Hiki ni kitu ambacho hakijazoeleka kusikika kwa Kiba hata kwa Diamond ila wanafanya hivyo kwa kazi maalumu.

Pili; katika Mediocre Alikiba anajiita Mtoto wa Kariakoo ambaye kwake ushamba ni mwiko, ukirudi kwenye Fresh Remix, Diamond anajiita Simba kutoka Mbuga ya Tandale. Hapa kila mmoja anajivunia mtaa anaotokea ndani ya Dar es Salaam, pia ndani ya mtaa kila mmoja ana kile kinachomtambulisha, sio kinyonge wala nini.

Tatu; kupitia Fresh Remix Diamond anajitambulisha kama Baba Tiffah na Nillan, halafu ukirudi kwa Mediocre, Alikiba anasema unaweza kumwita King Kiba, Baba Keyaan.

3. Kichupa cha kimtindo

Kwangu hii ni video ya pili kwa mwaka huu Bongo ambayo ipo ‘simple’ zaidi, ya kwanza ni ile ya Madee, Shenzi Type ambayo imepigwa ‘one take shot’ (bila kuunganisha picha) mwanzo hadi mwisho. Mediocre haina vitu vingi. Ina ‘scenes’ zisizozidi tatu.