Mchumba wa Davido akutwa na maambukizi ya corona

Muktasari:

Adedeji Adeleke maarufu Davido  ameamua kujitenga kwa siku 14, kuangalia kama yupo salama licha ya vipimo kuonyesha hana maambukizi hayo.

Staa wa muziki kutoka  Nigeria, David Adedeji Adeleke maarufu Davido  amewataka watu kutulia nyumbani ili kupambana na kuenea kwa virusi vya corona  (COVID-19).

Mkali huyo wa wimbo ‘Sweet in the middle’ ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa Instagram, mara baada ya kueleza jinsi mchumba wake Chioma Rowland alivyopata maambukizi ya virusi vya  corona.

“Tulia nyumbani, hatua hiyo itasaidia kupunguza kuenea kwa virusi hivi, kwa pamoja tunaweza kuimaliza corona,” ameandika Davido.

Awali, mmiliki huyo wa wimbo ‘Owo Ni Koko’, ameeleza mchumba wake huyo alivyopata  maambukizi ya virusi hivyo  baada ya kuchukuliwa vipimo  Machi 25,2020.

Staa huyo ameeleza hivi karibuni alirudi kutoka  Marekani ambako aliahirisha ziara ya kimuziki na mchumba wake aliyekuwa London nchini Uingereza naye alirudi pia.

Kutokana na historia ya safari zao, waliamua kupima ili kubainika kama wamepata maambukizi au la, baada ya vipimo vilivyohusisha watu 31 akiwamo mtoto wao, majibu yalionyesha Chioma amepata maambuzki.

“Watu wengine nikiwamo mimi na mtoto wetu, hatukukutwa na maambukizi, Chioma pekee ndiyo kakutwa nayo lakini pamoja na kukutwa na maambukizi hana dalili yoyote mpaka sasa.”

“Yupo katika uangalizi ingawa hana dalili yoyote, mimi pia nimejitenga kwa siku 14 ili kujisikilizia” ameandika Davido.  

Davido amewashukuru mashabiki wake na kumsihi kila mmoja kukaa nyumbani kwani hatua hiyo itasaidia kupunguza kuenea kwa virusi hivyo.