Mastaa Bongo Fleva waguswa na kifo Rais Mkapa

Muktasari:

Wasanii mbalimbali wameungana na watanzania katika kuomboleza kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa, aliyefariki usiku wa kuamkia leo Julai 24,2020

WASANII wa Muziki wa Bongofleva, wameshindwa kujizuia na kutumia mitandao ya kijamii kuonyesha namna gani ambavyo wameguswa na kifo cha Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.

Mkapa ambaye alizaliwa Novemba 12, 1938, aliiongoza Tanzania kwa miaka 10, kuanzia 1995 hadi 2005 amefariki Dunia akiwa Hospitali jijini Dar es Salaam akipatiwa matibabu.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond Platnumz aliposti picha ya Rais huyo na kuandika maneno mafupi kwa lugha ya kiingereza yaliyomaanisha, "Nafsi yake ipumzike peponi."

Upande wake Webiro Wassira maarufu kama Wakazi amesema amezipokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha Rais huyo.

"Mtu wa kanuni, dhamira thabiti na uadilifu hakika tutakukumbuka. Natoa pole kwa familia yake, marafiki, wanachama wa chama cha CCM, vile vile Tanzania nzima kwa ujumla."

Shilole hakuwa na mengi zaidi ya kusema kila nafsi itaonja mauti huku akitumia alama za mshangao kuonyesha hisia na kumalizia kwa kusema ‘Tangulia Baba’.

Zuchu alitumia maneno ya kiarabu kutokana katika kitabu cha Quran yasemayo, "Innalillah Wainna ilaih Raajuun," akiwa na maana sote ni wa Mungu na kwake tutarejea.

Mwana FA, ameonyesha kuguswa na kifo cha Mkapa kwa kusema ni habari mbaya na nzito, "Upumzike kwa amani mzee wangu Benjamin William Mkapa. Uliifanya vyema sababu ya uwepo wako duniani. Wewe ni somo kubwa kwenye maisha yetu watoto wako. MY LIFE MY PURPOSE."

Naye Barnaba Classic amesema,"Mungu yuko na baraka zake siku zote Tanzania. Tanzania ya leo hatuwezi zungumzia bila chembe ya mazuri yako Mzee Mkapa ulale salama mkono wa bwana akuponye, Amina R.I.P."

Msanii wa mashairi Mrisho Mpoto, amesema kifo cha Mkapa ni pengo kubwa na ni pigo kwa Taifa.

"Duh!! ngumu sana kuamini kwa haraka kama umetangulia, pumzika kwa amani kazi yako imeipa jina na heshima nchi yetu, umeenda ukiwa shujaa R.I.P Mzee Mkapa,"

Msanii wa kundi la Weusi G Nako ameandika kuwa ''Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa kiongozi wetu, mlezi wetu na Rais wetu mstaafu Benjamini Mkapa, salamu za pole ziwafikie ndugu jamaa na marafiki wa marehemu popote walipo, tuko pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu na Mungu awatie nguvu,"

Msanii mkongwe nchini, Lady Jaydee hakuandika chochote katika ukurasa wake badala yake aliweka picha ya Rais huyo.

Dogo Aslay aliandika; "Pumzika Kwa Amani mzee wetu Benjamini Mkapa”.

Naye Isha Mashauzi ambaye ni msanii wa nyimbo za taarabu, ameanmdika,”Pumzika kwa amani Rais wetu wa awamu ya tatu, tutakukumbuka daima’.

Rayvanny ameandika kwa maneno mafupi M.A.P.

Mwasiti naye hakuwa nyuma katika kuomboleza msiba huo mkubwa katika nchi kwa kuandika ‘Rest well,”.

Imeandikwa na Eliya Solomoni, Nasra Abdallah na Clezencia Tryphone