Martin Kadinda atwaa tuzo ya Mbunifu bora wa Kiume Afrika

Monday November 19 2018

 

MBUNIFU wa Kimataifa wa Tanzania, Martin Aloyce Kadinda juzi Jumamosi usiku alifanikiwa kutwaa Tuzo ya Mbunifu Bora wa Kiume katika mashindano yaliyofanyika mjini Lagos, Nigeria.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Jarida la Man la Nigeria yalifanyika sambamba na fainali za Mr. Universe, Kadinda aliwashinda, Ugo-Monye (Nigeria), Tokyo James (Nigeria), Sheria Ngowi (Tanzania), Kaijuka Abbasa (Uganda), Laduma na Baross wa Ivory Coast.

Katika shindano hilo lililofanyika kwenye hoteli ya hadhi ya nyota tano ya Oriental, Kadinda pia alizindua mavazi yake mapya yaitwayo ‘Shababy.’

“Kwa kweli najisikia furaha kuiwakilisha nchi yangu na kurudi na tuzo hii, mchuano ulikuwa mkali lakini Mungu amenisadia nimeweza kuchomoza kati ya wabunifu wengi wakubwa Afrika.

“Nawashukuru walionipigia kura kutoka nyumbani, tuzo hii iwe changamoto kwa wabunifu na vijana wengine waweze kufanya kile wanachokiamini.

“Siku zote nimeweka ubunifu kuwa ndio kazi yangu na nimekuwa nikijitahidi kutengeneza vitu vya kuvutia leo hii Afrika imenitambua, naamini baada ya hapa hata kwenye tuzo nyingine za dunia nitawika,” alisema.

Kadinda anakuwa mbunifu wa kwanza kutoka Tanzania kutwaa tuzo hiyo. Alianza kuwika baada ya kutengeneza makoti yaliyofahamika kama ‘Single Button’ na kuvaliwa na wasanii mbalimbali kama Diamond Platnumz, Hemed PHD, na kupata umaarufu katika maharusi.

Milango ikaanza kufunga na kupata nafasi ya kushiriki Tamasha la Music on the Catwlk lililofanyika Marekani kabla ya kwenda Nigeria. Martin anatarajiwa kurejea nchini wiki hii.

Advertisement