Maharusi washindwe wenyewe

Muktasari:

Mkurugenzi Mtendaji wa Adorable Wedding Trade Fair,  Ana Lema amesema maonyesho hayo ambayo sasa ni mara ya tatu kufanyika yanawahusisha watu wote wanaoandaa kuanzia shughuli za nguo za maharusi, washehereshaji (MC), Madjs, mapambo, wauza kadi, vyakula, keki, siku za kumbukumbu ya kuzaliwa na mambo mengine yanayohusisha sherehe kwa ujumla.

MAONYESHO ya Adorable Wedding Trade Fair yanaendelea kwenye ukumbi wa Mlimani City huku burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii wa kuigiza zikitolewa huku maharusi wakipewa ofa bab'kubwa.
Maonyesho hayo ambayo yameanza jana Ijumaa yanamalizika kesho Jumapili yanatarajia kuonyesha huduma zote za harusi ikiambatana na burudani za vichekecho kutoka kwa wasanii mbalimbali wa fani hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Adorable Wedding Trade Fair,  Ana Lema amesema maonyesho hayo ambayo sasa ni mara ya tatu kufanyika yanawahusisha watu wote wanaoandaa kuanzia shughuli za nguo za maharusi, washehereshaji (MC), Madjs, mapambo, wauza kadi, vyakula, keki, siku za kumbukumbu ya kuzaliwa na mambo mengine yanayohusisha sherehe kwa ujumla.
Amesema tofauti na maonyesho hayo, wameandaa shughuli nyingine kutakuwa na droo itakayowahusisha bibi harusi na bwana harusi wanaotarajiwa kuoana kuanzia Mei hadi Agosti..
"Unachotakiwa kufanya ni kwenda kuzunguka mabanda yote, hao watu watatoa kuponi kwenye mabanda hayo itakayosaidia kuingia kwenye droo na mshindi atatangazwa siku ya Jumapili ambapo zawadi ni kufanyiwa sherehe ya harusi yao bure ukumbi wa Kisenga,  watapewa watunza kumbukumbu (Photography na video camera), gauni la bibi harusi na suti ya bwana harusi, keki, mapambo na mahitaji mengine ya harusi," alisema .