Mabe.. Mabe.. Mabe.. Maberaa… (1949-2020)

Wednesday September 30 2020

 

By Kalunde Jamal

KATIKA moja ya nyimbo kali za Bendi ya Msondo Ngoma kwenye miaka ya hivi karibuni ni Ajali. Huu ni utunzi wa marehemu TX Moshi William uliotamba mwaka 2016/2017 na mpaka sasa haujachuja. Achana na mistari mikali inayosisimua na ujumbe wa TX na sauti za kina Maalim Gurumo, Maina, Hussein Jumbe, Karama Regesu na Romario au mbwembwe za Ally Rashid.

Kuna mtaalam mmoja wa kupiga gitaa la solo. Ametembea kwenye solo humo ndani mwanzo mwisho na kudhihirisha utamu wake kina TX, Gurumo na wakongwe wengine wa Msondo wakati huo walishindwa kujizuia wakatumia sekunde kadhaa kutukuza jina na umahiri wake wakimba...”Mabe..mabe..mabee…maberaaa...” Huyu ni mkongwe Said Mabera, ambaye usiku wa kuamkia jana alifumba macho na kuamua kuagana na dunia hii. Aligoma kabisa kuliona tena gitaa na kutii amri ya Alah kwenda kuanza maisha yake mapya peponi. Dah! Pumzika Mabera, fundi ambaye gitaa lilikutii. Mashabiki wako walipenda kukuita Dokta kutokana na umahiri wako. Hata pamoja na Meneja wa bendi Said Kibiriti kuthibitisha safari yake ya mwisho bado mashabiki wake haswa wa Ilala na mitandaoni walikuwa hawaamini mpaka jana jioni walivyompumzisha kwenye nyumba yake ya milele.

Mabera alikuwa nguzo imara ya Msondo tangu enzi na enzi na ameshikiri katika nyimbo zote kali za Msondo hata akaendelea kuwa kisiki baada ya wakongwe kama kina TX, Gurumo, Suleiman Mbwembwe na wengine kutangulia mbele za haki. Sasa na yeye ameamua kuwafuata.

Amedumu kwa miaka 48 bila kuhama Msondo tangu alipojiunga nayo Juni mwaka 1973. Hakuamini kwenye kuhamahama zaidi aliheshimu ofisi yake iwe wakati wa shida ama raha.

Bendi hiyo awali iliyokuwa inamilikiwa na Chama cha Wafanyakazi imepitia majina mengi ikiwemo NUTA Jazz, JUWATA Jazz, OTTU Jazz na sasa Msondo Ngoma.

Haya ni mahojiano yake ya mwisho na Mwanaspoti mwaka 2013;

Advertisement

Mabera anasema kuwa alijiunga na bendi hiyo mwaka 1973, wakati huo ikiitwa NUTA Jazz.

Hata hivyo, kwenye bendi hiyo alipelekwa na Mnenge Ramadhani (ambaye kwa sasa ni marehemu), baada ya kukutana naye mkoani Kigoma ambako wote ndio nyumbani.

“Nilikubali kuja Dar lakini kabla ya kuajiriwa na NUTA, niliamua kwenda Arusha na kufanya kazi kidogo kwenye Bendi ya Orchestra International iliyokuwa chini ya Amini Mussa,” anasema Mabera.

Anasema alipofika Dar es Salaam alikuwa anaishi kwa mjomba wake Hashim Rungwe maeneo ya Magomeni Mapipa Mtaa wa Kizingo, wakati huo akiwa na mke lakini kwa kuwa alikuja kwa mara ya kwanza alimwacha nyumbani Kigoma.

Mabera anasema mkewe huyo wa kwanza Mbega Shabani alikutana naye hukohuko Ujiji, Kigoma ambapo alikuwa jirani yao na kuamua kufunga naye ndoa na kubahatika watoto watano.

Baadaye akaoa mke wa pili mwaka 1982, ambaye waliachana na sasa (enzi hizo mwaka 2013) ana mke mwingine Mayasa Semkiwa waliyefunga ndoa mwaka 2000 na kwa wake wote hao amepata watoto 12. Alianza muziki mwaka 1961, kwa kujifunza gitaa maeneo ya Gungu, Kigoma ambako mwalimu aliyemfundisha alikuwa akipiga gitaa la solo kwenye Bendi ya Lake Jazz iliyokuwa Ujiji Kigoma.

Mabera anasema mwaka 1967 alijiunga na Bendi ya Lake Jazz na mwaka 1969 alijiunga na Tabora Jazz Band, iliyokuwa chini ya Mzee Mlekwa. Mwaka 1970 aliingia Musoma Jazz Band iliyokuwa ikiongozwa na Mzee Matiku, iliyokuwa na makazi yake mjini Musoma.

SIRI YA KUDUMU MSONDO

Mabera anasema moja ya sababu iliyomfanya adumu muda mrefu Msondo ni; “Nimekaa kwenye bendi hii kwa miaka mingi na ninaamini sisi ndiyo mizizi tunayoshikilia bendi hii kongwe hivyo, nikihama kama hivyo na Maalimu Gurumo amestaafu ina maana ni kulazimisha bendi ife wakati ina uhai mrefu. Sioni sababu ya kufanya hivyo nitadumu nayo hadi mwisho wangu kuwa mwanamuziki kama alivyofanya Gurumo.”

Anasema siku yake ya kwanza kuonyesha makali ilikuwa Ukumbi wa Amana Social Club na kupiga kwa umahiri mkubwa na ilipofika Juni 3 mwaka 1973, aliajiriwa rasmi NUTA na kuanza kuonyesha makeke yake kwa kupiga gitaa kwenye vibao kama ‘Maisha ya Taabu na ‘Nisinge kukimbia’.

Mabera anaeleza kuwa katika kazi ya muziki ametunga vibao vingi lakini ‘Mwana Acha Wizi’ na ‘Uzuri si Shani’ vilimpatia sifa na aliona hasa amekomaa kimuziki. Vibao hivyo alivitunga wakati ambao bendi hiyo imebadili jina na kuitwa JUWATA. Anasema hakuishia hapo kwani wakati bendi hiyo ikibadili jina na kuitwa OTTU Jazz, alitunga vibao vikali kama ‘Kifo cha Baba’ ambayo ilijumuishwa na nyimbo nyingine katika albamu ya ‘Binti Maringo’ na kutunga pia kibao cha ‘Huna shukurani’ kikibeba jina la albamu.

Mabera anasema amepiga gitaa kwa umahiri mkubwa lakini anaposikia wimbo ‘Faurata’, ambao ni utunzi wa Joseph Lusungu, hujiona kama hakuwa yeye kwa jinsi alivyofanya vitu kwa ubora wake.

“Nikisikiliza Faurata hujisikia kuwa hapo nilitimiza ndoto zangu za kuwa mpiga gitaa mahili nchini,” alisema Mabera.

Anasema pamoja na kupiga kwa umahiri gitaa la solo, mwanamuziki mwingine anayepiga kifaa kama hicho anayemvutia ni Miraji Shakashia wa African Stars ‘Twanga Pepeta.

“Kijana huyu (Shakashia) ananivutia sana kwa sababu anafanya kazi yake kwa umahiri mkubwa, naweza kusema kuna vitu navipata kutoka kwake,” anasema Mabera.

KIFO CHAKE

Mabera Said ambaye ni mtoto wa mwamuziki Said Mabera, alisema ni muda sasa walikuwa wakimuuguza baba yao kwa ugonjwa huo lakini juzi Jumatatu saa 11 jioni hali yake ilibadilika na kulazimika kumpeleka hospitali ya Massana iliyopo Mbezi Beach kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo, saa 3 usiku, hali yake iliimarika na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

“Tukiwa nyumbani baada ya saa kama mbili hivi hali yake ilibadilika tena presha kupanda na hapo ndipo umauti ulipomkuta wakati tukiwa tunafanya utaratibu wa kumrudisha hospitali,” alisema na kuongeza walimzika jana saa 10 makaburi ya Goba, jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Msondo, Said Kibiriti anasema taarifa za kifo cha Mabera walizipata asubuhi ya jana na ziliwashtua sana.

Kibiriti alisema katika kipindi cha miezi mitatu ya karibuni Mzee Mabera alikuwa akiumwa hadi kushindwa kushiriki naye katika maonyesho. “Magonjwa yaliyokuwa yanamsumbua zaidi ni kisukari na shinikizo la damu,” alisema.

PUMZIKA KWA AMANI SAID MABERA ‘DOKTA’. Muziki wa Tanzania utakukumbuka.

Advertisement