MTIKISIKO: Ulikuwa mwaka wa huzuni na mzuka tu

Muktasari:

Jamii ya Kitanzania kutokana na kuifuatilia burudani, imeshuhudia mengi mwaka huu na hadi tukikaribia kuufunga, Mwanaspoti limekuwekea baadhi tu ya matukio yaliyotikisa na kuteka hisia za watu.

IKIWA tunakaribia kuuaga mwaka 2018, yapo mambo mengi yamepotea. Kuna yaliyosahaulika na ambayo bado yapo mioyoni mwa wengi kutokana na ukubwa wa tukio lenyewe. Kuna yale ya furaha na huzuni lakini kwa namna moja yaligusa hisia za watu hasa kwenye upande wa burudani ambako, kumekuwa na mashabiki wengi. Iwe ni Bongo Movie au Bongo Flava na burudani nyingine.

Jamii ya Kitanzania kutokana na kuifuatilia burudani, imeshuhudia mengi mwaka huu na hadi tukikaribia kuufunga, Mwanaspoti limekuwekea baadhi tu ya matukio yaliyotikisa na kuteka hisia za watu.

NDOA YA KINA KIBA YAFUNIKA

Hawa ni ndugu wawili damu. Ali kiba na Abdukiba kwa pamoja waliamua kuachana na ukapera na kufunga ndoa. Alianza Ali kiba msanii mwenye jina kubwa nchini na nje ya nchi. Kimuziki amejitanua zaidi na hilo limemfanya ateke mashabiki wengi wanaofuatilia kazi zake na kile anachokifanya.

Kabla ya kuingia kwenye ndoa, Ali kiba, alidaiwa kuw ana uhusiano na Jokate Mwegelo wengi walikuwa wanategemea siku moja watafunga pingu za maisha kutokana na kuwa katika penzi la siri, lakini baadaye Kiba akawafanyia sapraizi Watanzania baada ya kufunga ndoa na Amina Khelef kutoka pale Mombasa, Kenya.

Ndoa hiyo ilizua hoja kwa upande wa upinzani ‘Team Diamond’ kutokana na upande huo umekuwa kama ukichukua chombo na kukitema kuliko kutulia, lakini pia wadau waliamini, Kiba angemuoa Jokate lakini haikuwa hivyo tena.

ALI KIBA AFUNIKA HADI HUKO

Inafahamika Ali Kiba anaupenda mchezo wa soka, lakini hakuna ambaye alikuwa anajua kuwa itatokea siku akajiunga kwenye soka la kulipwa na kukipiga Ligi Kuu.

Awali, aliwahi kutajwa kujiunga na African Lyon, lakini baadaye ikatajwa upande wa maslahi ndio ukamfanya Kiba aachane kabisa na masuala ya soka la Bongo.

Lakini msimu huu amewashangaza mashabiki wake wa muziki kwa kusajiliwa na Coastal Union, huku wadau wakijiuliza atawezaje kujigawa katika masuala yake ya muziki na soka.

Hata hivyo, Kiba akapeleka udhamini wa kinywaji chake MO Faya katika klabu hiyo na ndipo ikafahamika alikuwa yupo kibiashara kwa sababu hajawa karibu sana na timu hiyo tangu asajiliwe.

Pia, msanii huyu ameamua kuufungwa mwaka kitofauti kwa kuachia ngoma mfululizo yeye binafsi pamoja na kundi lake kitu ambacho alikuwa hakifanyi awali.

WASAFI YALETA MAPINDUZI

Miaka ya 2003 mpaka 2010 wasanii wengi walikuwa wanataka kujikomboa kwa kuanzia vitu vyao na kuachana na kutegemea tamasha kubwa moja tu nchini. Wapo waliojaribu na kutengwa lakini Joseph Mbilinyi Mr II au Sugu alijaribu kwa kuanzisha Kundi la Anti Virus ambalo lilionekana kuleta mapinduzi.Hata alipofanya tamasha lake katika Viwanja vya Ustawi wa Jamii alifanikiwa kujaza, lakini baadaye akapotezea harakati na kujiingiza katika siasa.

Lakini kwa upande wa Wasafi waliamua kuanza na channel yao ya televisheni na baadaye wakafungua stesheni ya Wasafi FM ili kujaribu kuwasogeza karibu wasanii ambao walikuwa na changamoto ya kutopigiwa nyimbo zao kwenye baadhi ya stesheni hapa nchini.

Kubwa zaidi ni mwezi Novemba walipoanzisha tamasha lao la Wasafi Festival, walijikusanyia wasanii mbalimbali nchini hadi ambao walikuwa hawapati nafasi ya kufanya shoo katika matamasha mengine. Huku tamasha hilo likionekana kuwa kubwa na kuteka hisia za mashabiki wengi kwa uchanganyaji wa wasanii kupamba steji moja.

FIESTA YAKWAMA DAR

Fiesta ndio tamasha kubwa na maarufu zaidi nchini, ambalo hufanyika nchi nzima kila mwaka. Ndio tamasha ambalo hukusanya wasanii wengi wa ndani na nje kwenye jukwaa moja na limedumu kwa miaka mingi huku kilele chake kila mwaka kikifungwa jijini Dar.

Kwa mwaka huu pia lilianza vizuri kwa kuzunguka mikoani, lakini wakati linataka kufikia kilele chake, mambo yakabadilika baada ya kunyimwa kibali na Ofisa Utamaduni Manispaa ya Kinondoni na waandaji kuamua kusitisha.

Hii inakuwa mara ya kwanza Fiesta kushindwa kufikia kilele chake huku Wasafi Festival likiendelea kuchanja mbuga kwenye mikoa mbalimbali nchini. Hapo maneno mengi yalizungumzwa kwenye mitandao ya kijamii mambo ndio yalikuwa moto zaidi.

Hata hivyo, limepangwa kufanyika Jumamosi ijayo Desemba 22 baada ya kushindwa kufanyika awali.

LULU ATOLEWA MAHARI

Elizabeth Michael ‘Lulu’ amekuwa akipitia katika misukosuko tangu kifo cha staa wa zamani wa Bongo Movie, Steven Kanumba mwaka 2012 kutokana na kukutwa na hatia na kifo hicho. Lulu alikuwa karibu na kuta za gereza kwa muda mwingi. Mwaka huu alitolewa na mwezi Novemba alijikuta akitembelewa na neema, baada ya mpenzi wake, Dj Majizo kumvisha pete ya uchumba na kumtolea mahari.

Hili ni tukio kubwa katika upande wa burudani kwa sababu hakuna, ambaye alikuwa anategemea kuona kama msanii huyo aliyeanza kutamba akiwa bado kinda ataveshwa pete muda mfupi baada ya kumaliza kutumikia kifungo chake cha nje.

SHOO KIBAO

Mwaka huu umekuwa na faida kubwa kwa wasanii kutokana shoo kuongezeka tofauti na mwaka jana ambao wasanii wengi walikuwa wakitegemea shoo kubwa ya Fiesta.

Mwaka huu wasanii wamejiongezea nafasi ya kufanya shoo kama Fiesta, Wasafi Festival, Kiba Tour na Shoo za EFM ‘Mziki Mnene’, hata wale ambao walikuwa wanakosa kupanda majukwaani katika shoo zilizokuwepo awali mwaka huu walipata nafasi.

DARASA TENA

Msanii huyu ambaye alitamba na wimbo wake wa Muziki, alikaa kimya kwa muda mrefu huku kukiwa hakuna taarifa kamili ni kitu gani ambacho kinaendelea kati yake. Watu mbalimbali walikidai amejiingiza katika vitendo haramu, lakini mwezi huu wa Desemba ameibuka na kukata mzizi wa fitna uliokuwepo awali na ameachia ngoma zake mbili ‘Achia Njia’ na ‘Tofauti’ huku mapokezi yake yakionekana kupokelewa vizuri na mashabiki waliokuwa wamemmisi.

BABU SEA AACHIWA

Familia ya Nguza Viking ilikuwa nyuma ya kuta za Gereza la Ukonga takribani kwa miaka 10, lakini mwaka huu ulikuwa wa neema kwao baada ya Rais John Pombe Magufuli, kutoa msamaha na kuwaachia huru Nguza Viking na Papii Kocha.

Familia hiyo baada ya kuachiwa huru ilikaa kimya kwa muda wa mwezi mmoja kisha ikaachia ngoma ya ‘Waambie’ na ulifanya vizuri kabla ya kuanza kufanya shoo kwa kuzunguka mikoani.

WASANII KUTIKISWA BASATA

Baraza la Sanaa Tanzania liliwaita na kuwahoji baadhi ya wasanii ambao walikuwa na visanga mbalimbali ambavyo vilikuwa na picha tofauti mbele ya jamii. Roma Mkatoliki, Wasafi, Nay wa Mitego na wengineo, walikuwa wakipishana katika milango ya ofisi hizo zilizopo katika mitaa ya Ilala kwenda kutatua matatizo waliyokuwa wanakabiliwa nayo. Majanga hayo pia yamemkuta Wema Sepetu, ambaye mpaka sasa bado yuko kifungoni akitekeleza agizo la Bodi ya Filamu Tanzania.

Miss Tz yarejea

Mwaka jana Desemba shindano la Miss Tanzania lilifutwa, lakini mwaka huu lilirejeshwa na kufanikiwa kumpata Miss Queen Elizabeth ambaye alienda kutuwakilisha katika mashindano ya kimataifa. Hata hivyo, hajafanya vizuri katika mashindano hayo licha ya kuonekana kuwa tishio kwa washiriki wenzake.

KIFO CHA MASOGANGE

Mwaka huu, licha ya matukio ya kufurahisha, tasnia hii pia ilikumbwa na matukio ya huzuni baada ya kukumbwa na misiba iliyofululiza.

Masogange alikuwa ni miongoni mwa ma-video Queens ambao waliotamba nchini kutokana na mwonekano wake kuanzia juu mpaka chini na alikuwa hayumbi anapokuwa mbele ya kamera. Lakini, ghafla alizua simanzi kubwa baada ya mauti kumfika Aprili kwani, aliteka hisia za watu wengi waliokuwa hawaamini kile ambacho walikisikia.

Katika msiba wake pia ulifichua kabisa usiri uliokuwepo kwenye uhusiano wa staa wa Bongo Movie, Irene Uwoya na Mbongo Flava, Dogo Janja, kwani baada ya msiba huo kutokea Mwanspoti lilishuhudia wawili hao wakiishi katika mjengo (apartment) ambayo alikuwa anakaa pia marehemu Agnes Masogange.

Kifo cha Masogange kitabaki kuwa pengo kwa upande wa Ma-video Queen, kutokana na kwamba alikuwa na umbo fulani hivi la kipekee kitu ambacho hivi sasa kinakosekana hali ambayo inafikia kutumia wadada kutoka Afrika Kusini.

MZEE MAJUTO

Msanii Nyandu Tozi aliwahi kuimba moja ya nyimbo zake “Bongo hakuna Supastaa kama King Majuto,” hiyo ilitokana na jamaa alikuwa anapendwa na kujulikana nchini hadi nchi za jirani.

Uwezo wake wa kumfanya aliyenuna kuanza kucheka mwenyewe halikuwa jambo dogo hata kidogo. Wapo wachekeshaji wengi ambao wana uwezo huo lakini Majuto alikuwa noma.

Yaani hata ukimwangalia tu basi unajikuta unacheka.

Lakini, mwezi Julai Watanzania walipata tarifa za kifo chake na kujikuta wote wakiinamisha vichwa chini kwani, taarifa hizo zilishtua mpaka viongozi wa juu serikalini kutokana na ukaribu wao na watu hao.

PATRICK WA MUNA LOVE

Msiba wa mtoto wa msanii Muna Love, Patrick uliteka hisia za watanzania wengi kiasi cha kuufanya msiba huo kugeuka kuwa mkubwa nchini na kwenda kufanyika katika Viwanja vya Leaders, sehemu ambayo inafanywa misiba ya watu maarufu kutokana na wingi wake.

Msiba huu pia ulitikisa mitandaoni kutokana na kuibuka kwa ugomvi wa kugombea nani ni baba halali wa mtoto huyo. Mama wa mtoto, Muna Love alidai baba wa mtoto ni mwingine na mwanaume mwingine alijitokeza na kudai yeye ndiye baba wa mtoto.Pia, Muna Love aliingia kwenye ugomvi mzito na familia yake na baadhi ya wasanii wenzake pia kutokana na msiba huo kuwa sehemu mbili.