MDORORO: Mfumo ndio unakosesha soko tasnia ya filamu

Muktasari:

  • Kuna wakati wanalalamika wasanii ambao ndio watayarishaji na wanaohusika na uchanguzi wa wasanii (Casting Director) kutaka kucheza hata zile nafasi ambazo hawaendani nazo, si ajabu mtu akataka kucheza kama mtoto japo hana sifa hizo.

TAKRIBAN miaka mitatu hali ya soko la filamu linasuasua huku kukiwa na taarifa zinazokingana na uhalisia.

Wapo wanaosema tasnia ya filamu inazidi kukua na wale ambao wanashuhudia kuanguka kwake lakini kila amesalia na jibu lake kichwani

Jambo hili linakosesha wadau na wapenzi wa filamu majibu sahihi lakini wengi wakisalia kuangalia tamthilia ya Kifilipino na Kikorea ambazo zina ubora mkubwa lakini suala la maudhui usiniulize kwani kila Taifa lina utamaduni wao ambao ndio Uzalendo.

Tatizo kubwa kwetu ni mfumo wa uandaaji wa filamu hadi kuingia sokoni si mfumo rafiki, tunajaribu kwenda kisasa lakini mawazo yetu sokoni ni ya kizamani, hapa ndipo penye changamoto kubwa, huwezi kukimbizana na utandawazi na mambo ya teknolojia miundombinu dhaifu.

Ubora wa kazi

Ubora wa kazi zetu umelalamikiwa sana na wadau wa filamu ambao ndio wateja wenyewe lakini hakuna aliyejali hapa wanaohusika ni wasambazaji ambao walitengeneza mfumo wa kuangalia sura badala ya uwezo wa waigizaji, yaani kuwapangia watayarishaji, kurudia hadithi wasanii wale wale.

Kila filamu inapotoka huwezi kuona kuacha kukutana na sura zile zile Jb, Muhogo Mchungu, Riyama Ally, Hashim Kambi, Hemed Suleiman, Yusuf Mlela, Irene Uwoya, Jack Wolper, na majina yanayorindima lakini bado wasanii hawa wamebaki katika uhusika ule ule.

Hata hivyo, kwa sasa soko linaongozwa na wasanii wawili tu ambao ndio hata wakichezeshwa katika filamu mbaya wanauwezo wa kuuza filamu yako, ni Salim Ahmed ‘Gabo Zigamba’ na Riyama Ally ambaye anawakilisha kidadada, si dalili nzuri

Kuna wakati wanalalamika wasanii ambao ndio watayarishaji na wanaohusika na uchanguzi wa wasanii (Casting Director) kutaka kucheza hata zile nafasi ambazo hawaendani nazo, si ajabu mtu akataka kucheza kama mtoto japo hana sifa hizo.

Tozo

Watayarishaji na wasanii wanalalamika kuhusu tasnia ya filamu kuwa na matozo mengi bila kuangali hali ya soko mfano mtayarishaji mmmoja analalamika kwa kusema kibali cha kuandaa filamu ni pesa za Kitanzania lakini tano, ukaguzi wa filamu kwa kila dakika ni Sh1,000.

Pia kuna gharama nyingine kutoka Cosota ambazo ni lazima ulipe bila kujali unazo au hauna kwani ni sehemu ya kulinda haki yake, kuna gharama za Mamlaka ya mapato, bado gharama za uandaaji ni kubwa ambazo kwa sasa si rahisi kurudisha.

Bei ya sokoni kwa sasa ni laki tano ndipo unatakiwa kujiuliza je wasanii hawa na watayarishaji wanalipanaje na kuweza kuendelea kuigiza?

Angalia gharama zinazomkabili mtayarishaji na msanii mwenyewe ambaye ndio mhusika mkuu.

Tumefeli wapi?

Nadhani ni katika mfumo wa uuzaji filamu. Ni wazi kwa sasa mfumo wa uuzaji wa filamu duniani huanza na majumba ya sinema, uuzaji wa Televisheni, mitandao na mwisho ndio uuzaji wa Dvd ambao kwetu ndio njia kuu, hatuwezi kufika popote kwa staili hii ambayo tumeing’ang’ania kuishikilia na kubaki na taarifa zisizo na usahihi. Inabidi tujipange upya kwenda kisasa.